Vijana wapatiwa mafunzo kuhusu mfumo wa Taarifa za soko la ajira

Baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa watafutaji kazi kuhusu mfumo wa Taarifa za soko la Ajira kwa Wilaya za Unguja wakimsikili za mgeni rasmi (hayupo pichani)katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliofanyika katika ukumbi wa hospitali ya Wagonjwa wa akili Zanzibar.

 

Mkurugenzi Ajira kutoka Wizara ya Kazi,Uwezeshaji, Wazee, Vijana na Watoto Ameir Ali Ameir akitoa hotuba ya makaribisho kwa mgeni rasmi katika mafunzo kwa watafutaji kazi kuhusu mfumo wa Taarifa za soko la Ajira kwa Wilaya za Unguja yaliofanyika katika ukumbi wa hospitali ya Wagonjwa wa akili Zanzibar.

 

Baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa watafutaji kazi kuhusu mfumo wa Taarifa za soko la Ajira kwa Wilaya za Unguja wakimsikiliza mgeni rasmi (hayupo pichani) katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliofanyika katika ukumbi wa hospitali ya Wagonjwa wa akili Zanzibar.

 

Mgeni Rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Shamata Shaame Khamis akitoa hotuba ya Ufunguzi katika mafunzo kwa watafutaji kazi kuhusu mfumo wa Taarifa za soko la Ajira kwa Wilaya za Unguja yaliofanyika katika ukumbi wa hospitali ya Wagonjwa wa akili Zanzibar.

 

Mmoja kati ya washiriki wa Mafunzo kwa watafutaji kazi kuhusu mfumo wa Taarifa za soko la Ajira Ahmed Abdalla Nassor akitoa shukurani kwa mgeni rasmi baada ya kuwafungulia mafunzo hayo yaliofanyika katika ukumbi wa hospitali ya Wagonjwa wa akili Zanzibar.
PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR.

ILI kumaliza malalamiko ya ajira kuchukuliwa na wageni, ni lazima vijana wa Zanzibar wabadilike na kujiendeleza zaidi kielimu.

 

Aidha, wametakiwa kuutambua vyema mfumo mpya wa taarifa za soko la ajira uliopo katika Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto na kuutumia katika kutafuta nafasi za kazi katika taasisi na kampuni mbalimbali.

 

Akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusiana na mfumo huo yanayofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Afya hospitali ya Kidongochekundu,  Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Shamata Shaame Khamis, amesema huu si wakati wa kulalamika bali ni wa kujipanga.

 

Katika mafunzo hayo yaliyoshirikisha vijana wa Wilaya ya Magharibi ‘B’, Shaame ameeleza kuwa tatizo la uhaba wa ajira haliwezi kumalizwa na mtu, taasisi au jumuiya moja moja, bali linahitaji nguvu za pamoja ili kulitatua.

 

Kwa hivyo, ameishukuru Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuona umuhimu wa kuwashirikisha vijana wa Zanzibar katika mradi wa mafunzo hayo unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika (ADB).

 

Amefahamisha kuwa, mfumo huo wa taarifa za soko la ajira ni muhimu katika kuwaunganisha waajiri na watafutaji kazi, sambamba na kuongeza kasi ya upatikanaji wa fursa za ajira kwa vijana nchini.

 

Hata hivyo, amewatahadharisha vijana kutokubali kudanganywa na watu wanaodai wana uwezo wa kuwapatia kazi serikalini iwapo watatoa fedha.

 

Amesema watu wanaofanya hivyo ni matapeli na hawapaswi kuachiwa kujinufaisha kwa mgongo wa vijana wanaotoka katika familia za kimasikini kwa kisingizio cha kuwakomboa kiajira.

 

Shaame amesema serikali imeweka idara na utaratibu maalumu wa kushughulikia utoaji wa ajira kila kunapojitokeza haja ya kufanya hivyo na wala haitumii mawakala katika kuorodhesha vijana wanaosaka ajira.

Shaame alieleza kuwa, ukosefu wa ajira kwa vijana ambalo ni tatizo la dunia nzima, unachangia kukosa kipato kwa jamii, jambo linalodhoofisha uwezo wa matumizi na hivyo kuwaingiza baadhi ya watu katika madeni na vitendo vyengine visivyofaa.

 

Katika kulipatia ufumbuzi tatizo la ajira, Naibu Waziri huyo alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikipanga mikakati maalumu kuwawezesha vijana, pamoja na kushirikiana na wahisani mbalimbali wa ndani na nje katika kubuni nafasi za kazi ikiwemo ujasiriamali.

 

Akitoa mada katika mafunzo hayo yaliyoshirikisha vijana 45 wa Wilaya ya Magharibi B, Mkurugenzi wa Ajira Ameir Ali Ameir, amesema wakati umefika vijana wanaomaliza masomo wasichoke kujiendeleza kielimu ili waweze kukubalika katika soko la ajira.

 

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa uwelewa wa mfumo huo, changamoto zake na namna watakavyoweza kukabiliana na waajiri wanapokwenda kutafuta kazi.

 

Huo ni muendelezo wa mafunzo ambayo hivi karibuni yalifanyika katika Wilaya za Wete na Chake Chake kisiwani Pemba, lengo likiwa kuzifikia wilaya zote 11 za Zanzibar.

 

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

10 JUNI, 2017