Dk. Shein akutana na madaktari kutoka China

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa utamaduni wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China wa kuendelea kuleta Madaktari kila baada ya miaka miwili ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar sambamba na kukuza uhusiano na ushirikiano mwema kati ya nchi mbili hizo.

 

Dk. Shein aliyasema hayo  leo Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo kati yake na  Madaktari wapya pamoja na wale wanaomaliza muda wao kutoka Jamhuri ya Watu wa  China, wakiongozwa na Balozi Mdogo wa nchi hiyo anayefanya kazi zake hapa Zanzibar  Balozi Xie Xiaowu.

 

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa utamaduni wa nchi hiyo wa kuleta Madaktari kwa ajili ya kutoa  huduma za afya hapa Zanzibar ni wa kihistoria ambao umeanza tokea mwaka 1964 na kuendelea hadi hivi leo ambapo China ilianza kuleta wataalamu wake mbali mbali  hapa Zanzibar wakiwemo Madaktari.

 

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wa Zanzibar wanathamini na wanazipenda huduma zinazotolewa na Madaktari kutoka nchini China ambao wamekuwa wakishirikiana vyema na Madaktari wazalendo kutoa huduma hizo kwa ufanisi mkubwa hapa Zanzibar.

 

Pia, Dk. Shein, alitumia fursa hiyo kueleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar huku akiahidi kuendelezwa na kudumishwa na kusisitiza kuwa  China imeweza kutoa mchango mkubwa katika mafanikio ya sekta ya afya na  sekta nyengine mbali mbali hapa Zanzibar ikiwemo sekta ya viwanda, elimu,kilimo, michezo, habari na nyengienzo.

 

Dk. Shein aliwakaribisha Madaktari hao wapya hapa Zanzibar na kuwaaga wale waliomaliza muda wao huku akieleza matumaini yake makubwa kuwa madaktari hao wapya kuwa watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi kama wenzao wanao ondoka ambao wamefanya kazi vyema katika kutoa huduma za afya.

 

Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Madaktari 21 wanaomaliza muda wao kwa kusaidia kutoa huduma mbali mbali za afya ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi kwa vitendo yakiwemo mafunzo ya upasuaji na matumizi ya mashine mpya katika hospitli ya Mnazi Mmoja ikiwemo mashine mpya za kisasa (TURP), zikiwemo upasuaji wa matatizo ya mkojo pamoja na tiba ya njia ya mfumo wa chakula pamoja na huduma nyenginezo.

 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China chini ya kiongozi wake Rais Xi Jingping kwa kuendelea kuisaidia na kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo hapa Zanzibar.

 

Akitoa pongezi hizo, Dk. Shein alisema kuwa Rais Xi Jingping ameweza kutekeleza makubaliano yote aliyoahidi kuisaidia Zanzibar ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee pamoja na vifaa vyake ambao tayari umekamilika, ujenzi wa uwanja wa Maotsetung, ujenzi wa Bandari mpya ya Mpigaduri, ujenzi wa jengo jipya la abiria katika kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume na miradi mengineyo.

 

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimueleza Balozi mdogo huyo wa China kuwa ipo haja kwa China kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kuendeleza sekta ya afya kwa kuunga mkono uendelezaji wa kitengo cha saratani, kitengo cha maradhi ya mkojo na vigo pamoja na uanzishwaji wa kitengo cha upasuaji wa moyo ili huduma hizo ziweze kutolewa hapa hapa Zanzibar ambapo tayari baadhi ya huduma hizo zimeshaanza kutolewa.

 

Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa juhudi ilizoanza kuchukua Serikali katika kuviimarisha vitengo hivyo ni kutoa mafunzo kwa madaktari wachache wa vitengo hivyo pamoja na baadhi ya vifaa lakini hata hivyo alisisitiza haja ya kuungwa mkono  ili kuongeza nafasi zaidi za masomo kwa ajili ya madaktari na wataalamu wa kada hizo, vifaa na mambo mengineyo hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika kada hizo.

 

Nae Balozi Mdogo wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Balozi Xie Xiaowu alimueleza Dk. Shein kuwa  timu ya  26 ya Madaktari kutoka  nchini China inayomaliza muda wake imefanya kazi vyema na kuahiadi timu ya 27 nayo itafuata nyayo hizo hizo kwa kufanya vizuri sambamba na kuhakikisha inatoa ushirikiano mkubwa kwa wananchi, madaktari wazalendo pamoja na viongozi wa Serikali.

 

Balozi Xie Xiaowu alimuhakikishia Dk. Shein kuwa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi yake ya maendeleo sambamba na kuimarisha uchumi wake kwa kutambua kuwa nchi mbili hizo zinaurafiki na udugu wa miaka 53 tokea Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.

 

Nae kiongozi wa Madaktari hao waliomaliza muda wao, Dk. Xu Zhuoqun alitoa pongezi kwa mashirikiano mazuri aliyoyapata kutoka kwa viongozi wa Serikali, madaktari wazalendo pamoja na wananchi wakati wote walipofanya kazi zao hapa Zanzibar huku wakiwasifu watu wa Zanzibar kwa ukarimu wao mkubwa.

 

Nao Madaktari wapya chini ya kiongozi wao Dk. Wang Hao, walitoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa makaribisho na mapokezi mazuri waliyoyapata hapa nchini na kuahidi kutoa ushirikiano wao kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Unguja na Pemba katika kutoa huduma ya afya.

 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk