BoT: D9 Club inafanya ushawishi wa ununuzi wa hisa bila vibali vya mamlaka husika

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) zinapenda kuutahadharisha umma kwamba, taasisi ijulikanayo kama D9 Club inayotangaza au kushawishi, pamoja na mambo mengine ununuzi wa hisa, inafanya hivyo bila vibali vya mamlaka husika.

Ni imani ya BoT na CMSA kuwa ushawishi unaofanywa na D9 Club kwa umma kushiriki katika mpango wao utasababisha watu kupoteza fedha zao, na pia ni kinyume na Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania ambayo katika Fungu la 171A,171B na 171C, ni kosa la jinai kuendesha, kushawishi watu kushiriki, na kushiriki au kuchangia fedha katika upatu.

Ifahamike kwamba upatu haramu hubuniwa kwa namna ambayo fedha za kila mshiriki mpya hutumika kumlipa mshiriki aliyetangulia, na hakuna maelezo ya namna yoyote ya kuwekeza au kuzalisha fedha hizo.

Kwa taarifa hii, umma unasisitizwa kutoshawishika kwa namna yoyote ile kushiriki katika upatu uliobuniwa na D9 Club na mipango mingine ya aina hiyo. Aidha, wananchi watoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika, ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana na vyombo vya usalama (Polisi) kuhusiana na mikutano au mafunzo yanayoendeshwa na D9 Club na mipango mingine haramu kama inayofanana na huo.

Imetolewa na:

BENKI KUU YA TANZANIA & MAMLAKA YA MASOKO YA

MITAJI NA DHAMANA

14 Juni 2017