SMZ ya shauriwa kuwa na mikakati maalum ya kupambana na mfumko wa bei za vyakula

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshauriwa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha uzalishaji wa ndani unaongezeka ili kupunguza tatizo la kupanda kiholela mfumko wa bei za bidhaa hususani za vyakula.

Akisoma taarifa ya kamati ya Bajeti,kuhusu makadirio ya mapato na Matumizi ya bajeti ya serikali ,muelekeo wa uchumi na mapango wa maendeleo kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo katika kikao cha Baraza la wawakilishi Chukwani.

Mjumbe wa kamati hiyo Abdallah Ali Kombo amesema mfumko wa Bei Zanzibar umepanda hadi kufikia asilimia 6.7 mwaka 2016,kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka 2015 kutokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula siku hadi siku.

Amesema Zanzibar ikijitahidi kuimarisha uzalishaji wa ndani itapunguza kuagiza vyakula kutoka Tanzania Bara na nje ya Nchi na hivyo kusaidia  kuwapunguzia wananchi usumbufu wanaoupata wakati wakihitaji huduma muhimu za chakula hususani katika kipindi hichi cha mwezi wa Ramadhani.

Akizungumzia suala la misamaha ya kodi kwa wafanya biashara kamati hiyo imeomba serikali kuwafatilia ili kuwachukulia hatua wafanya biashara waliopewa misamaha hiyo na kushindwa kuitumia kwa kutoa huduma nafuu kwa wanunuzi wao wakiwemo wananchi wa kipato cha chini.

Amesema mbali na serikali kuzisamehe Fedha nyingi za  kodi zilizokusudiwa kukusanywa ili kuimarisha maendeleo ya nchi ,lakini imeonekana fedha hizo kuwanufaisha Wafanya biashara peke yao,kinyume na matarajio yaliokusudiwa ikiwemo kupunguza bei kubwa ya bidhaa zao kwa wananchi wa kipato cha chini.

Na:Fat hiya Shehe Zanzibar24.