Mdadi wa sherehe za sikukuu, usivunje sheria za barabarani

MWISHONI mwa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani, waislamu duniani kote, huungana pamoja kuadhimisha sikukuu ya Eidel-fitry.

Waislamu, baada ya kutimiza mfungo huo, kisheria hulazimika kusherehekea sikukuu hiyo, kwa kula, kunywa na kuvaa vizuri tena imesisitizwa viwe vya halali.

Yapo mambo kadhaa ndani ya siku hiyo, yamekatazwa kisheria kuyafanya, ikiwa ni pamoja na kufunga, kunywa ulevi, zinaa, kufanya kazi ingawa kwa kipindi maalum.

Ingawa kila tendo linalopelekea dhambi, limeshapigwa vita na kupingwa vikali na maandiko matakatifu, lakini siku hiyo ya sikukuu yamesisitizwa zaidi, kuyaacha.

Yapo pia yaliogogotezewa kufanywa ndani ya sikukuu, kwamba yanaongeza sunna zaidi, ikiwa ni pamoja na kutembelea wagonjwa, kuwasaidia wasiojiweza, kuwatembelea ndugu na jamaa hasa waliokaribu.

Ingawa kwa mtindo usiokubalika, wapo wanaosherehekea sikukuu hiyo kwa kupanda magari yalioruhusiwa kubeba abiria 20, ingawa huanzia 30 hadi 45 wengine wajirusha kwa mwendo kasi .

Inawezekana wanafanya hivyo, kama sehemu ya sherehe, ingawa wanajua kuwa, kwenye uislamu hakuna sherehe ilioruhusiwa kwa kuvunja sheria hata kama ni za nchi, maana haziathiri uislamu.

Suala la kuheshimu sheria za nchi, linamgusa kila mmoja, na wala ujio wa sikukuu hii ilioko mbele yetu, haijaruhusu na wala haina mamlaka ya kuwataka vijana na wazee wa kiislamu, kuvunja sheria za usalama barabarani.

Walishasema wataalamu wa sheria na wanazuoni, kuwa kila kitu kinachofanywa, ni vyema ikaangaliwa sheria kwanza, kwa hapa Tanzania na Zanzibar kuelekea sherehe hizi za sikukuu, hilo linapaswa kuliangaliwa.

Lazima ujiulize suali, tena ni vyema na kujitafutia na jibu wewe mwenyewe, kama umeshafunga mwezi mzima wa ramadhani ukiamini kuwa kufanya hivyo ni wasjibu, sasa je kuvunja sheria za usalama barabarani unadhani ni sunna.

Mwendo kasi, kupakia watu zaidi ya uwezo wa gari, ulevi na kisha kuendesha gari, gari za mizigo kufanywa ndio za kubebea abiria, unadhani haya ni sahihi.

Kwa mfano, sheria ya uchaguzi ya Zanzibar no 11 ya mwaka 1984, kwenye kifungu chake cha 56, kimehalalisha suala la vyama kufanya kampeni, ingawa sio kwenye nyumba za ibada.

Kumbe nalo hilo lipo kisheria, kama kilivyo kifungu cha 7, kinavyoeleza haki ya kupiga kura kwa mzanzibari alietimiza masharti kwa mujibu wa sheria.

Kama kila jambo linafuata sheria, iweje kipindi cha sikukuu wazazi na walezi kuwaruhusu hasa watoto na vijana wao, kujazana pomoni kwenye magari kama vile sheria ya usalama barabarani imeenda likizo.

Kwa hili la kuvunja kwa sheria ya usafiri barabarani, kwa waislamu kwa kisingizio cha kusherehekea sikukuu, na kisha kujazana kama makumbi kwenye gari, mbona hufanywa kama vile sheria au katiba imeridhia.

Ingawa juzi Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Sheihan Mohamed Sheihan, wakati akizungumza na ukurasa huu, alishatamka kuwa mara hii wapiganaji wake watakua makini na hilo.

Iweje kwenye nchi moja sheria nyengine ziwe makini kusimamiwa na hata wananchi wenyewe, mfano kumpiga bakora aliegundulika kula mchana wa ramadhani, lakini hili la kuvunja sheria barabarani liwe baridi.

 “Katika hili jeshi la Polisi, halitaangalia mtu usoni, gari inayobeba abiria 20 ikizidisha, taratibu za kisheria zitafuata  mkondo wake, maana wengi wanadhani, kipindi cha sikukuu kama vile sheria hazipo’’,alisema.

Kama kila kitu kinapaswa kifanywe kwa mujibu wa sheria, ni lazima sheria ya usalama barabarani ya Zanzibar no 7 ya mwaka 2003, ifuatwe kikamilifu, maana hili ni kwa maslahi ya watu wote.

Lakini jeshi hilo katika sherehe hizo za sikukuu, limeaapa kupambana na wale wanaoendesha vyombo vya magaurudumu mawili, kwa mwendo kasi “tako moja’.

“Hawa ndio wamekuwa wachafuzi wakubwa wa sheria za barabarani na kupelekea wanaosherehekea kujaa na hofu ya usalama, sasa lazima tutawaangali mara mbili”,alisema Kamanda.

Kama katiba ni sheria mama, basi ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Ibara yake ya 13, na ya Zanzibar kifungu cha 12 vimetamka, lazima kuwe na usawa mbele ya sheria, iweje kipindi cha sikukuu usalama barabarani uwe rehani.

Na ndio maana Jeshi la Polisi mkoani wa kusini Pemba, likaenda mbali na kuvitaka vyombo vyengine vinavyosimamia, kuwa gari iliosajiliwa kwa ajili ya kubeba mizigo, yatatiwa mkononi ikiwa yatagundulika kubebea watu kwenye siku zote za sherehe.

“Tumegundua hata magari ya aina hiyo hubeba watu kupindukia, hivyo inapotokea ajali, hata idadi ya wanaoumia au kufariki huwa kubwa’’,alisema kamanda wa Polisi.

Mwananchi Aisha Hassnuu Omar (30) mkaazi wa Wawi Pemba, anakumbuka vyema mwaka juzi, kulipotokezea ajali eneo la Chanjamjawiri, baada ya gari iliobeba vijana waliokuwa wakitokea kwenye sherehe za sikukuu na kupinduka.

“Mimi naona jeshi la Polisi kipindi cha sikukuu kama wanaopata mapumziko ya kazi zao, kwanini wanaona gari ya abiria imejaa kupindukia lakini hawaisimamishi’’,alihoji.

Bimkubwa Haji Ali (29) wa Chake chake, anasema sheria za usalama barabarani, hutakiwa kusimamiwa wakati wote, ingawa Polisi kipindi cha sikukuu huachia wenye magari wafanye watakavyo.

Dereva wa gari ya abiria Said Haji Kombo (30) anaebeba abiri Chake chake – Wete, anashangaa kuona siku za kawaida abiria mmoja akizidi, dereva na kondakta wake hufikishwa mahakamani, ingawa wakipeleka watu  kwenye sherehe za sikukuu hawaulizwi.

“Sisi madereva hata abiria wakijazana kiasi gani hatuathiriki, maana pesa inaongezeka, lakini kazi ya kupekua na kuhesabu abiria, polisi waifanye vipindi vyote’’,alishauri.

Kondakta wa gari ya Mkoani- Chake Ali Muhusin, yeye anadhani kipindi cha sikukuu, kama vile askari wa usalama barabarani wamepewa tamko la kuzisamehe gari za abiria na wajaze wapendavyo.

Sheria no7 ya Zanzibar ya mwaka 2003 ya usafiri barabarani, imetamka makosa kadhaa ambayo mtu akiyafanya atakua ni mkosaji, kwa mfano kuzidisha abiria.

Sheria inaelekeza dereva akizidisha abiria aliosajiliwa kwenye gari yake, adhabu yake ni kutoza faini ya dola 10 za marekani, sawa na wastani wa shilingi 1,400, sambamba na dola 5 kwa kila abiria aliezidi.

Ingawa sheria ikafafanua kuwa, kama hilo ni kosa la pili, sasa faini itakuwa dola 15, kwa kila abiria aliezidi, ambapo ufafanuzi kwa abiria aliezidi ni yule aliekaa chini.

Sasa kwenye kipindi cha kuelekea sikukuu, wapo madereva huruhusu gari zao, kupakia watu hadi juu ya bodi, ingawa sheria ya usafiri barabarani ipo saa 24.

 

HAJI NASSOR OUT, PEMBA.