Kesi ya Halima Mdee yakamilika

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee (39), anadaiwa kumtukana Rais kwa kusema kuwa “Rais Dk. Magufuli anaongea ovyo ovyo, anatakiwa afungwe breki”.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana iliambiwa kwamba upelelezi wa kesi ya Mbunge huyo kwa tuhuma za kumtukana Rais Magufuli tayari umekamilika.

Baada ya taarifa hiyo, mahakama hiyo ilipanga kusikiliza maelezo ya awali Oktoba 11, mwaka huu.

Madai hayo yalitolewa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Mutalemwa Kishenyi, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Victoria Nongwa.

Kishenyi alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana na kwamba upelelezi umekamilika.

Alidai kuwa upande wa Jamhuri unaomba tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali.

Hakimu Nongwa alisema mahakama yake itasikiliza maelelezo ya awali Oktoba 11, mwaka huu.

Awali, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, akisaidiana na Mwendesha Mashtaka, Inspekta wa Polisi Hamisi Said, ulidai kuwa Julai 3, mwaka huu, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, katika ofisi za Makao Makuu ya Chadema, mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo.