Mapambano yaendelea dhidi ya Zitto Kabwe na Spika Ndugai

Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya Chama Cha ACT Wazalendo Mh. Zitto Kabwe ameendelea na Spika wa Bunge Job Ndugai na kusema kuwa ameibuka na sakata lake yeye ili kutaka kufunika nguvu ya wananchi kuhoji juu ya kupigwa risasi  tundu Lissu.

Zitto Kabwe amesema hayo leo mara tu baada ya Spika wa Bunge Job Ndugai leo bungeni kusema anauwezo wa kumzuia Mbunge huyo asizungumze bungeni hadi mwisho wa bunge hilo kwani Zitto hawezi kupambana naye.

“Nimegundua Spika Ndugai ameibua mashtaka yangu ili kufunika ufuatiliaji wa wananchi kuhusu Tundu Lissu kupigwa risasi. Nimeamua sitawapa hilo” aliandika Zitto Kabwe kupitia mtandao wake wa Twitter

Kwa upande wake Spika Ndugai  amesema Zitto Kabwe hawezi na hapaswi kujibizana naye, na kumtaka Zitto Kabwe kutomfananisha na aliyekuwa Spika wa Bunge marehemu Samuel Sitta, kwani hawezi kufanana naye na kila mtu ana muda wake, kama ambavyo Spika wa bunge aliyepita mama Anna Makinda alivyokuwa na muda wake kuliongoza bunge hilo.

Spika Ndugai  jana aliagiza Mbunge Zitto Kabwe na Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea kufika kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili kuhojiwa kutokana na kauli walizotoa hivi karibuni, nae Zitto Kabwe kamjibu spika huyo kuwa mambo anayoyafanya Spika yanaporomosha bunge.