Uchunguzi shambulizi la Tundu Lissu, Familia yakinzana na CHADEMA

Familia ya Tundu Lissu imesema wao hawana mashaka na jeshi la polisi kufanya uchunguzi juu ya tukio lilomkuta ndugu yao ingawa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, kikisisitiza uchunguzi ufanywe na vyombo vya kimataifa nasio jeshi la polisi.

Wakili Alute Mughwai ambaye ni kaka wa Tundu Lissu ametoa kauli hiyo huko jijini Arusha na kusema mpaka sasa wanaimani na uchunguzi unaofanywa na jeshi la polisi na iwapo familia itakaa kwa mara nyingine kuzungumzia suala hilo na kuja na kauli nyingine ya pamoja kama familia wataamua ni nani afanye uchunguzi wa tukio hilo kama kutakua na ulazima wa kufanya hivyo.

“Hatujakaa sisi kama wanafamilia kutoa msimamo wetu kuhusiana na uchunguzi wa tukio hilo, kwamba hatuna imani na jeshi la polisi na uchunguzi ufanywe na vyombo vya kimataifa lakini kama tukikutana tukawa na msimamo wetu tutatoa maoni yetu kama haja itakuwepo,” amesema Mughwai.

Hivyo amelitaka jeshi la polisi kuanzia uchunguzi wao kwa kufuatilia mkutano aliokuwa akizungumzia suala la Bombadier kukwama nchini Canada na alipozungumzia suala la kufuatiliwa na watu asiowafahamu.

Hata hivyo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema jana kilisema kinahitaji serikali iruhusu wachunguzi wa kimataifa kuingia nchini kufanya uchunguzi juu ya shambulio la kupigwa risasi kwa  Mbunge na Mwanasheria wao Tundu Lissu mnamo Septemba 7 mwaka huu mchana eneo la ‘Area D’ mjini Dodoma.