Wanne washikiliwa wakielekea kujiunga na kundi la kigaidi Al-Shabaab

Watu wanne wanaoaminika kuwa raia wa Burundi wameshikiliwa na polisi nchini Kenya baada ya kugundulika walikuwa wakielekea Somalia kujiunga na kundi la al-Shabaab .

Msemaji wa Polisi George Kinoti, amebainisha kuwa Maafisa wa ujasusi walikuwa wakiwafuatilia washukiwa hao baada ya kupata habari kuhusu mipango yao ya kwenda kujiunga na kundi la Al-Shabaab.

Amefafanua kuwa washukiwa hao wanne walikamatwa katika kizuizi cha polisi mjini Isiolo takriban kilomita 350 kaskazini mwa mji mkuu wa nairobi wakielekea katika mji wa mpakani wa Mandera.

Maafisa wa polisi pia wanasema wanne hao waliingia nchini Kenya kama watalii kupitia visa huru ya ushirikiano kati ya Burundi na Kenya.

Maafisa katika Ubalozi wa Burundi mjini Nairobi wanasema kuwa watatoa taarifa kamili kuhusu kukamatwa huko baada ya kushauriana na mamlaka ya Kenya.

Mnamo mwezi Januari mwaka huu raia mwengine wa kigeni, ambaye alikuwa Mtanzania alikamatwa mjini Mandera akijaribu kuvuka na kuingia Somalia kwa lengo la kujiunga na kundi hilo la al-Shabaab.