Rakhine mpaka Bangladesh: Siku 7 za kuwabeba wazazi wake mabegani mwake

Wakimbizi wa kabila la Rohingya wanamiminika katika nchi ya Bangladesh kutokana na vipigo kutoka kwa jeshi la Myanmar huku ikiwabidi kusafiri safari yenye uchungu wakipita katika vilima na mito. Vichaka, mashamba na misitu imekua vitanda kwa maelfu ya watu wanaovuka mpaka kuelekea Bangladesh tangu vurugu za kikabila zilipoanza mwezi uliopita magharibi mwa Myanmar.

Wakionekana katika hali ya dhiki kubwa, moja ya picha yenye kuumiza mioyo imeenea katika mitandao ya kijamii. Picha hiyo inamuonesha kijana wa kiislam wa Rohingya akiwa amewabeba wazee wake, Mama yake na baba yake katika vikapu alivyovibeba kwenye mabega yake ili kuondoka nao kutoka katika mji wa Rakhine.

Katika umri ambao alitakiwa kuwa skuli akisoma au kazini, kwake yeye ni tofauti amejikuta akipaswa kubeba mzigo katika mabega yake na kusafiri nao umbali unaokadiriwa kufikia maili 100.

Kijana huyo amesema hakuweza kuwaacha wazee wake hao, hivyo aliamua kuwabeba kwenda nao Bangladesh, huku akitembea bila viatu kwa siku saba.

Inakadiriwa zaidi ya wakimbizi 370,000 wamekimbilia Bangladesh tangu August 25 vita vya kikabila vilipoanza magharibi mwa Myanmar katika jimbo la Rakhine .