Wanafunzi wa kike watakiwa kuwa na msimamo  na mbinu za kujipatia elimu

Mtayarishaji wa Tamasha la  filamu ZIFF  Robert Monondolo amewataka  Wanafunzi  kuwa na bidii, msimamo  na mbinu za kujipatia elimu ili kupata muongozo wa maisha yao ya  baadae.

Amesema wanafunzi waepukane na vishawishi ambavyo vitawapelekea kuwaharibia maisha yao ya baadae na kuweza kuyahatarisha  kwa kujiingiza katika mambo ambayo bado muda wao haujafikia.

Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Muyuni Jendele na Ndijani wakitizama filamu ya faraja iloandaliwa na wataarishaji waTamasha la filamu ( ZIFF ) wakishirikiana na Jumuiya ya kumuendeleza Mtoto wa kike Masomo ya Sayansi katika mradi wa tuseme.

Hayo aliyasema huko katika Skuli ya Sekondari ya  Muyuni B wakati alipokuwa akionesha filamu kwa wanafunzi wa sekondari ya Muyuni Jendele na Ndijani katika  mkoa wa kusini Unguja.

Alifahamisha lengo la kuonesha filamu hiyo ni kuweza kuwazindua wanafunzi ambao bado wako finyu kimawazo katika kujipatia elimu na kuona jinsi mwanafunzi faraja alivyoonesha msimamo wake wa kujipatia elimu bila kujali shindikizo la wazee kwa kumuozesha mume mapema.

Filamu hiyo imeandaliwa na Jumuiya ya kumuendeleza mtoto wa kike masomo ya sayansi  ( FAWE) wakishirikiana na watayarishaji Tamasha la filamu (ZIFF) ikiwa ni moja ya kuwafanya wanafunzi waweze kusema na kujiamini .

Nao wanafunzi hao walieleza matatizo mbali mbali ambayo yamo katika vijiji vyao ikiwemo muamko mdogo wa wazee juu ya kumuhamasisha mtoto kupata elimu .

Wakieleza athari ambazo zinawapata pindi wakilazimishwa kuozeshwa katika umri mdogo ni kupoteza damu nyingi ,kupata kifafa  cha uzazi hatimae kusababisha kifo.

“Tunakosa haki zetu za msingi wazazi  hawana elimu ya kutosha kujua nini thamani ya elimu kwa mtoto ndio chanzo cha kutuamulia kutupa waume katika umri mdogo na kutusababishia matatizo, “ walisema wanafunzi  hao.

Jumuiya ya kumuendeleza mtoto wa kike masomo ya sayansi  ( FAWE ) imeandaa mafunzo maalum kwa wanafunzi  wa mjini na vijijini  ili kuwafanya waweze kusema pindi wakinyimwa haki zao za msingi .

Na Khadija  Khamis.