Ndege yaanguka katika Ziwa Nakuru Kenya

Ndege moja aina ya helikopta imeanguka katika ziwa Nakuru nchini Kenya muda mfupi baada ya kuondoka katika hoteli moja mjini humo.

Afisa mkuu wa Polisi mjini Nakuru Joshua Omukata amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa walikuwa wakisubiri boti kufanya operesheni ya kuwanusuru waliokuwa ndani ya ndege hiyo ambapo ripoti zinasema kuwa kulikuwa na watu watano katika ndege hiyo.

Seneta wa Nakuru Susan Kihika amesema kuwa watatu kati ya watu waliokuwemo katka ndege hiyo walikuwa wanachama wa kitengo chake cha mawasiliano.

Ndege hiyo iliondoka katika hoteli ya Jarika County Lodge na duru zinasema kuwa ilikuwa ikipaa chini chini kabla ya kuanguka.

Ndege hiyo ilitarajiwa kusafirisha waandishi wa habari katika mkutano wa kampeni .

Waokoaji walikuwa bado hawajaanza operesheni saa nne baada ya ndege hiyo kuanguka katika ziwa hilo kwa ukosefu wa boti.

Waokoaji walilazimika kusubiri boti kusafirishwa kutoka Ziwa Naivasha.

Mkurugenzi wa Idara ya kitaifa ya kukabiliana na majanga Pius Masai amesema kuwa ndege ya polisi imetumwa katika eneo hilo kusaidia katika uokoaji.