JUMAZA yapinga matakwa ya Asasi za kiraia

Jumuiya ya maimamu Zanzibar JUMAZA imesema hairizishwi na matakwa ya asasi za kiraia juu ya kutaka awepo kadhi mwanamke katika Ofisi ya kadhi Zanzibar kwa lengo la kutetea haki za Wanawake.

Akizungumza na Zanzibar24 ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar ,Katibu mtendaji wa JUMAZA Shekh Muhidin Zubeir amesema hakuna sheria ya dini ya kiislamu inayoruhusu kuwepo kwa kadhi mwanamke hivyo si vyema kwa asasi za kiraia kulazimisha suala hilo.

Amesema ni vyema jumuiya hizo kujikita katika kazi walizokusudia  ikiwemo kusimamia masula ya udhalilishaji yanayoendelea katika jamii na kujiepusha na mambo yatakayo haribu amani Nchini.

’’Watendaji wa jumuiya asasi za kiraia tumieni elimu mulizonazo katika kusaidia jamii hususan katika masuala ya udhalilishaji na sio kukimbilia ukadhi kwa wanawake jambo ambalo halileti taswira nzuri katika dini ya kiislamu’’

Aidha amesema JUMAZA itendelea kusimamia haki na wanawake  hususani katika kesi za  mirathi na ndoa ili wanawake wa kiislamu waweze kunufaika na haki zao za msingi ambazo wanazikosa katika familia zao.

Hata hivyo ametoa wito kwa asasi za kiraia kufuata mila na desturi za kizanzibar katika utendaji wao wa kazi pia ametoa wito kwa Serikali  kulichunguza kwa kina suala hilo na kulichukulia hatua za kisheria  kabla suala hilo halijaleta migogoro ya uvunjifu wa amani katika jamiii.

Akizungumzia suala la kamati iliyounganisha Jumuia ya Maimamu na Jumuia ya asasi za kiraia amesema kamati hiyo haitakuwepo tena na kutowa wito kwa jamii kuendelea kupeleka kesi zao sehemu husika ili ziweze kupatiwa ufafanuzi.

Hivi karibuni Jumuiya ya asasi za kiraia iliitaka serikali kubalidi mfumo wa uteuzi wa makadhi ili kuruhusu makadhi wanawake waweze kuhudumu katika mahakama za kadhi ikiwa ni juhudi za kuondosha ubaguzi wa kijinsia katika kusimamia haki za wanawake na watoto.

Na;Fat-hiya Shehe Zanzibar24.