RC Ayoub: Wakaazi wa tumbatu rejesheni umoja wenu ilikuleta maendeleo

KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, amewaomba wakaazi wa kisiwa cha Tumbatu kurejesha umoja waliokuwa nao awali, ili maendeleo zaidi yaweze kupatikana.

Ushauri huo aliutoa wakati akizungumza na wananchi wa shehia za Tumbatu, katika ziara yake ya kuyatembelea maeneo mbalimbali ya mkoa huo yenye lengo la kusikiliza kero za wananchi.

Alisema muda mrefu wakaazi wa kisiwa hicho wamekuwa wakitofautiana na kusababisha maendeleo kudumaa, hivyo kuna haja ya kuweka pembeni tofauti hizo na kufanya kazi pamoja kwa umoja wao.

Alisema masuala ya siasa, yamewafanya wakaazi wa kisiwa hicho kusambaratika, lakini akawambia kuwa siasa ni mambo yanayokuja na kupita, lakini umoja na mshikamano utabakia daima hasa ikizingatiwa wote ni ndugu wa mama na baba mmoja.

Aidha alisema historia ya kisiwa hicho inaonesha wakaazi wake ni wamoja, hivyo kuna haja umoja huo kuendelezwa na wasikubali kugawanywa kwa sababu ya tofauti za kisiasa.

“Tumetenganishwa wakati tushajitawala, wazee wangu nawaomba tusikubali kusambaratishwa, kwa sababu yoyote ile, sisi ni wamoja na daima tutaendelea kuwa wamoja, tujitathmini tulipokosea ili turekebishe,” alisema.

Aliwahimiza kuendelea kushirikiana kwenye shughuli za maendeleo na kijamii, kama harusi na maziko na kuacha kubaguana.

Alisema changamoto zinazokikabili kisiwa hicho zitaondoka, kama wananchi watashirikiana na kamwe wasitarajie kwamba mtu kutoka nje anaweza kuja kutatua changamoto zao.

Nae Zubeir Bakari Ali mwananchi wa shehia ya Jongowe, alisema wamefarajika kumuona Mkuu wa Mkoa kufika katika kisiwa hicho kusikiliza matatizo yanayowakabili.

Hakika tunaandika tarehe muhimu sana na hii haifutiki maana hatujawahi kumuona kiongozi wa ngazi kama yako,” alisema.