Serikali inataka wanawake na maendeleo ili kufikia uchumi wa kati

Wanawake nchini  wametakiwa  kuwa tayari katika  kufanya kazi pamoja na kuzitumia  ipasavyo  fursa mbalimbali  za   kujiendeleza  kimaisha ili kwenda sambamba  na malengo ya serikali  ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

Akizungumza na Zanzibar24 Mratibu wa Kampeni ya kuhamasisha wanawake na  kutoa elimu ya kutengeneza  bidhaa mbalimbali za ujasiriamali Abla Mohammed Baraka amesema  kwa kiasi kikubwa  wanawake  wamekuwa wakichangia pato la taifa  hivyo  ni vyema kusimama imara katika kujiunga na  vikundi  vya ushirika ili waweze kujikimu na kuondokana na utegemezi.

Amesema utegemezi wa wanawake katika familia  unachangia kwa kiasi  kikubwa kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji  hivyo nivyema   kujiamini  katika kufanya shughuli za maendeleo ili kuweza  kujikwamua  na hali ngumu ya maisha.

Aidha Abla ameiyomba  Serikali kuendelea na juhudi zake za kutoa fursa kwa wanawake  za kuwapatia  mitaji  hasa katika vikundi vya  ushirika  ili waweze kujiendeleza  katika  kazi zao  kwani baadhi yao hushindwa  kutokana na kutokuwa na mitaji.

Kampeni  ya kuhamasisha  wanawake ijulikanayo kwa jina la wanawake  chakarika  imekuwa ikitoa elimu mbalimbali kwa wajasiriamali  ili waweze  kupata ujuzi zaidi  ikiwemo utengenezaji wa Sabuni za aina  tofauti na  utafutaji  wa masoko.

Amina Omar Zanzibar24