Serikali yawaonya wanaoshirikiana na OGP

Serikali imesema italivunja baraza la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ikiwa litaendelea kushirikiana na Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP) wa kimataifa ambao nchi imejitoa.

Onyo hilo lilitolewa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni mstaafu George Mkuchika alipokuwa anajibu swali la nyongeza lililoelekezwa wizarani kwake na Zitto Kabwe.

Katika kujenga hoja yake, Mbunge huyo wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), alisema nchi za Hungaria na Urusi ambazo Tanzania imefuata nyayo zake kujitoa kwenye mpango huo ni miongoni mwa nchi ambazo zinatuhumiwa kwa kuendeshwa bila misingi ya kidemokrasia na kidikteta hivyo ni aibu kwa Tanzania kuiga nchi hizo.

“Majukwaa haya ya kimataifa yanatengeneza ushawishi kwa sababu Mwenyekiti wa OGP ni Canada,” Zitto alisema, na “juzi Rais (John Magufuli) alisema serikali imemwandikia barua Waziri Mkuu wa Canada kuhusiana na suala la (kuzuiwa huko kwa ndege ya) Bombardier.

“Serikali haioni kwamba iwapo Tanzania ingekuwa imeendelea kuwa mwanachama wa OGP, ombi hili la Rais lingeshughulikiwa kwa uzito zaidi?”

Zitto alisema Manispaa ya Kigoma Ujiji ni miongoni mwa miji 15 ambayo inashiriki katika OGP kwa uhuru na haizingatiwi kwamba nchi ipo kwenye OGP au laa.

“Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na ushiriki si tu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ambayo inafaidika sana, lakini pia na miji mingine ambayo pia inataka kuingia kwenye OGP?” Zitto alihoji.

Katika majibu yake, Mkuchika alisema Tanzania ilipofanya uamuzi huo haikuiiga nchi yoyote bali ilifanya hivyo kwa kupima vigezo kwa kuzingatia ilivyoona inafaa kutokana na Tanzania ni taifa huru linalojitawala, linalofanya uamuzi wake lenyewe bila kushurutishwa na taifa lolote, liwe kubwa ama dogo duniani.

Aliongeza kuwa Tanzania na Canada ni wanachama wa Jumuiya ya Madola na Tanzania ina ubalozi Canada,hivyo kuwapo au bila kuwapo OGP, mawasiliano kati ya nchi hizo mbili hayawezi kuwa tatizo.

Mkuchika alisema andiko la OGP linasema nchi ikijitoa, washirika wake wote waliomo ndani ya nchi husika nao uanachama wao na shughuli zao zinakoma.

“Serikali inayotaarifa kwamba Manispaa ya Kigoma Ujiji mpaka sasa inawasiliana na OGP, na OGP wamemwandikia Waziri wa Mambo ya Nje kwamba wana nia ya kuendelea kushirikiana na Ujiji,” Mkuchika alisema na kufafanua zaidi:

“Nataka kutumia bunge kuionya Manispaa ya Ujiji, nchi inayozingatia utawala haiwezi kufanya maamuzi baraza la madiwani likasema ‘sisi ‘hatuta-comply’ (hatutayafuata), haitotokea.

“Nataka niionye Manispaa ya Kigoma, waache mara moja, watekeleze maamuzi ya serikali na wakiendelea kufanya mawasiliano kama wanavyofanya sasa, serikali itachukua hatua kali zaidi na hatua hizo kwenye manispaa ni kuvunja baraza la madiwani na kuweka tume ya manispaa.

“Nawaomba huko mlipo wa Kigoma na Zitto msiifikishe serikali huko.”

Katika swali la msingi, Zitto alihoji sababu za serikali kuamua kujiondoa kwenye mpango wa OGP.

Akijibu swali hilo, Mkuchika alisema OGP ulitokana na wazo la Rais wa Marekani, Barack Obama kwa lengo la kuzifanya nchi mbalimbali duniani kuwa wazi katika uendeshaji wa shughuli za serikali.

Alisema mpango huo ulizinduliwa kama taasisi isiyo ya kiserikali Septemba 20, 2011 na Tanzania ilijiunga Septemba 21, 2011 baada ya kukidhi vigezo vya kujiunga ambavyo ni pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora.

Alisema mpango huo ni wa hiari na nchi inaweza kujiunga baada ya kutimiza masharti na hata kujitoa bila kuwapo kwa kizuizi chochote.

Waziri huyo alisema kuwa hadi sasa, nchi wanachama wa OGP ni 70 na kati yao, 10 ni kutoka barani Afrika.

“Baada ya serikali kushiriki utekelezaji wa mpango kwa zaidi ya miaka minne imeamua kujitoa. Tanzania si nchi pekee iliyojiunga na mpango huo kisha kujitoa. Nchi nyingine ni kama Hungary (Hungaria) na Urusi ambazo zilijiunga na kujitoa baadaye,” alisema.

Mkuchika alisema serikali tangu kupata uhuru imekuwa na ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kutekeleza falsafa ya uwazi na uwajibikaji.

Alisema serikali imejiunga na kutekeleza mpango wa kikanda na kimataifa kama vile mpango wa nchi za Kiafrika wa kujitathmini katika nyanja za utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa (APRM).

“Ni maoni ya serikali kuwa shughuli zinazotekelezwa na kupitia vyombo hivyo zinatosha kwa nchi kuendelea kujijengea misingi imara ya uendeshaji wa shughuli za serikali kwa uwazi, kuongeza uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa,” alisema na kueleza zaidi:

“Nilihakikishie bunge kuwa Tanzania kujitoa katika mpango huo hakuna madhara yoyote. Mipango inayotekelezwa ndani ya nchi kama ilivyoelezwa inajitosheleza kuendeleza na kuimarisha misingi hiyo ya uwazi na uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.”