Kwa hili hongera ZAECA Pemba

Wiki iliopita Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Pemba, ilitoa taarifa ya mwenendo wa ulipaji wa fedha, baada ya wananchi kadhaa kukodi mikarafuu ya Serikali.

Maana wizara hiyo, ilikuwa ikiendesha zoezi la ukodishaji wa mashamba hayo, ambayo lengo baada ya kukodi ni kulipa fedha serikalini ili ziingie kwenye mfuko mkuu wa hazina.

Sihaba mashamba fedha kadhaa huwenda zikapatikana, iwapo waliokodi watalipa maana ni zaidi ya shilingi bilioni 2.5, ingawa hadi sasa kati ya hizo zilizoingia serikalini ni shilingi milioni 900.393.

Wakati hilo likiwa kwenye hatua, hiyo na Wizara ya Kilimo ikitaka kumaliza kuyakodisha mshamba ya serikali, ZAECA iliyaibua mashamba mengine 30.

Kwa hili ZAECA hongereni kwa kuyaibua mashamba 30 ya serikali, ambayo yanaamini mengine yalifichwa kwa makusudi, mengine kusahauliwa, ingawa ZAECA walifanikiwa kuyaibua.

ZAECA, inaonekena imedhamiria kweli kuuweka kwenye mazingira mazuri uchumi, maana imekuwa ikifanya kazi ya ziada, ili kuhakikisha serikali haiibiwi.

Mashamba haya 30 wala sio kidogo kwa kuyaokoa, maana inawezekana kuna mabwana wakubwa, pengine kwa makusudi walishayachupa kwenye zoezi la ukodishaji.

Lazima nirejee tena kwa maofisa wa ZAECA kuwapa hongera kwa kazi yao nzuri, ambayo naamini kila mpenda maendeleo basi kwa hili na jengine lazima alikubali.

Na ZAECA baada ua kuyaokoa mashamba haya, pia imesababisha kuingizia serikali zaidi ya shilingi milioni 84, kwa msimu huu baada ya kukodishwa.

Siunajua wizara ya kilimo ilikuwa kwenye mchakamchaka wa ukodishaji mashamba ya kimarafuu yake ya eka tatu tatu, basi taarifa zinaeleza hayo, 30 wapo walioyaacha ili baadae wayarudie kwa kuyachuma.

Inawezekana hilo, kwamba baadhi ya watendaji wakorofi tena ndani ya wizara ya Kilimo pengine kuyaficha kwa makusudi, maana wapo wanaojengwa na tamaa.

Kwani hukumbuki hao hao ZAECA, si walimtia mikononi mtendaji mmoja wa wizara ya Kilimo, kwa kotoa ushauri wa siri, na kisha kutengeneza kizuka bandia ili alipate shamba la mikarafuu.

ZAECA baada ya kupiga mbizi, walimgundua mtendaji huyo, ambae kwa sasa ameshatengenezewa jalada lake, kwa ajili ya kufikisha mahakamani.

Hongera za ZAECA ni kwa silimia 99, lakini 100 zote kwa kiongozi wetu mpendwa rais wa Zanzibar kwa wazo, fikra, ubusara wake wa kuanzisha taasisi hii.

Maana waliowengi wakati inazinduliwa, hawakuamini kwamba ingeweza kufanya kazi kubwa kama hii ya kuokoa mali za serikali, kuishia mikononi mwa wachache.

Kama ZAECA imeokoa shilingi 84, kwa msimu huu baada ya kuyafichua mashamba 30, kumbe kimehesabu sasa mikarafuu hiyo, itaendelea kuwa mikononi mwa serikali daima, napengine msimu ujao, fedha itakuwa kubwa.

Kama wizara ya kilimo, Wilaya, Mkoa au ZSCT wanatafuta taasisi iliotoa mchango mkubwa, katika kuukinga uchumi wa Zanzibar usipotee, basi si vibaya kuitupia macho ZAECA.

Kwa hili nasema tena hongera ZAECA, hongera maofisa wote kwa kazi nzuri na ya kufurahisha mlioifanya, kwenye zoezi la ukodishaji mashamba ya serikali kwa msimu huu.

Lakini nayi wizara ya Kilimo, endeleeni kufanya kazi pamoja na taasisi hii, kwa vile nanyi mnalengo la kuukuza na kuuendeleza mbele uchumi wa Zanzibar.

Jamii na makundi mengine lazima sote kwa pamoja, kuhakikisha tunazisaidia na kuzipatia taarifa rasmi taasisi kama ZAECA na nyengine ili, tujenge nchi yetu kwa pamoja.