Rais wa Zanzibar awahakikishia wananchi wa Michamvi huduma ya Maji

RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia wananchi wa kijiji cha Michamvi, kilichopo Mkoa wa Kusini Unguja kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa kipaumbele kufanikisha mradi wa maji safi na salama katika kijiji hicho na imelenga kuukamilisha ipasavyo katika kipindi kifupi kijacho.

 

Dk. Shein aliwataka wananchi wa kijiji hicho pamoja na viongozi wa Mkoa huo kuyachukua maelezo yake kuwa ndio sahihi na si maelezo yanayotolewa kinyume na hayo huku akisisitiza kuwa Wizara ya Fedha na Mipango imeshaagizwa ikimilishe miundombinu inayohitajika ili maji yawafikie wananchi wa Michamvi.

 

Dk. Shein aliyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa CCM wa Mkoa wa Kusini Unguja ulioenda sambamba na uchaguzi wa viongozi wa Mkoa huo Kichama, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Coconut, Marumbi, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

 

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa licha ya juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miaka ya sabini na thamanini kuyapatia maji maeneo ya Michamvi, ikiwemo  kuchimba kisima na mahodhi mawili, bado maeneo hayo yanakabiliwa na tatizo la maji.

 

Aliongeza kuwa sababu kubwa ni kuwa eneo hilo limekuwa na uwekezaji mkubwa wa mahoteli pamoja na maji matamu ya kisima kilichochimbwa awali kugeuka kuwa na chumvi nyingi.

 

Alieleza kuwa juhudi nyengine zimefanywa na Kampuni ya UST ya Ujerumani ambapo wametengeneza kituo kidogo cha kusafisha maji ya chumvi na kuwa maji matamu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), kituo ambacho kinatoa kiasi cha lita 800 kwa siku na kinatumia umeme wa nguvu za jua.

 

Hivyo, Dk. Shein alieleza kuwa katika kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika kijiji hicho, Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Ras al Khaimah, imechimba kisima maalum katika eneo la Ghana, Bwejuu kwa ajili ya kupeleka maji safi na salama kijijini huko.

 

Aidha, alieleza kuwa kipo kisima maalum kinachotoa huduma kwa wawekezaji, ili kuepuka upungufu wa maji katika kisima kinachotoa huduma kwa wananchi na kuongeza kuwa hadi sasa tayari tangi la ujazo wa lita laki mbili limeshajengwa na pampu inayohitajika imeshanunuliwa na kazi iliyobaki ni usambazaji wa mambomba na ufikishaji wa umeme.

 

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika la Umeme Zanzibar ZECO pamoja na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa kutekeleza maagizo yake vyema aliyoyatoa Agosti mwaka huu alipofanya ziara mkoani humo.

 

Dk. Shein alitoa agizo kwa ZECO kufikisha umeme katika kisima kilichopo Mwambiji ndani ya kipindi cha miezi miwili pamoja na kuitaka ZAWA ikamilishe kazi iliyobakia ili maji kwa maeneo ya Kibuteni na Makunduchi yapatikane haraka.

 

Alieleza kuwa kazi hiyo ilifanywa vizuri na taasisi hizo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira ambapo umeme ulifikishwa katika kipindi cha wiki mbili tu na ZAWA nayo ilikamilisha miundombinu iliyobaki kwa ufanisi mkubwa  na kueleza matumaini yake kuwa mapema mwezi ujao huduma hiyo itapatikana vizuri katika vijiji hivyo.

 

Dk. Shein alisisitiza kuwa utoaji huduma bora za jamii ni kipimo muhimu wanachotumia wananchi wakti wanapofanya tathmini na kupima utendaji wa Serikali pamoja na chama chake.

 

Hivyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa ni lazima viongozi wahakikishe kuwa wanaitekeleza kwa mafanikio makubwa mikakati imara ya kuziendeleza sekta hizo, ili kila wanapopima utendaji wao waridhike na watosheke na juhudi na mipango yao.

 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa matunda ya Mapinduzi ni kufanyika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, tarehe 26 April 1964 na kusisistiza kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na Muungano huo ni nguzo muhimu za Taifa zenye nguvu, mshikamano na umoja hivyo, zitaendelea kulindwa na zitadumu milele na kamwe hatoruhusiwa mtu kuzichezea.

 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk