Kikosi cha wapelelezi kutinga Nairobi kumhoji Tundu Lissu

Timu ya  wapelelezi ya Jeshi la Polisi imetumwa kwenda jijini Nairobi, nchini Kenya kufanya mahojiano na Mhe. Tundu Lissu kuhusu tukio la kushambuliwa kwake  pamoja na kumhoji dereva wake.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro ambaye amesema wametuma wapelelezi Nairobi baada ya kusikia Lissu amekubali kuhojiwa juu ya tukio hilo na matarajio yao pia ni kumpata dereva na mlinzi wake.

Tumetuma watu wetu kwenda kuchukua maelezo yake (Lissu)..Mwanzo tuliomba kwenda lakini chama (Chadema) walikataa. Juzi tumesikia wamesema wapo tayari…Tumetuma vijana wetu wawili kwenda Nairobi kuchukua maelezo yake.amesema IGP Sirro.

IGP Sirro amesema lengo kubwa la mahojiano ni kujua mazingira ya shambulio yalikuwaje na kwamba ikiwezekana wampate dereva na msaidizi huyo wa Lissu ili kurahisisha upepelezi wa tukio lenyewe.

Upelelezi unaingia vitu vingi sana (sasa) kutompata dereva na mlinzi wake Lissu inashindwa kutupa picha kamili ya tukio, alibainisha IGP Sirro huku akiwataka Watanzania kuwa na imani na jeshi la polisi katika kufuatilia tukio hilo.

Niwaambie Watanzania watuamini, hatuko kwa ajili ya kuona hatumtendei mtu haki, tupo kwa ajili ya kutenda haki.amesema IGP Sirro.

Tangu Mhe. Lissu ashambuliwe kwa risasi na watu wasiojulikana mwezi Septemba 7, mwaka huu mjini Dodoma, Polisi ilikuwa bado haijafanya mahojiano naye na hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na jeshi hilo ambalo awali lilikamata magari nane aina ya Nissan Patrol, meupe, yaliyokuwa kwenye viunga vya Dodoma siku ya tukio.