Mwanafunzi kidato cha tatu akamatwa na sare za Polisi (JWTZ)

Jeshi la Polisi Kanda Maalum DSM linamshikilia mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Said Selemani miaka 17 mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Fahari iliyopo Goba kwa kosa la kukutwa na sare za JWTZ (Kombat).

Mwanafunzi huyo alikamatwa huko maeneo ya Mbezi CRDB bank akiwa amevaa sare hizo za JWTZ huku akivuta sigara hadharani na kufanya vitendo vingine ambavyo haviendani na maadili ya askari aliyevaa sare.

Katika mahojiano ya awali kijana huyo alijitambulisha ni askari toka kikosi cha 501 KJ kilichopo Lugalo jijini Dsm,baada ya kubanwa zaidi alikiri kupata uniform hizo toka kwa rafiki zake anaokuwa nao sehemu mbalimbali.

Aidha alipopekuliwa katika begi la mgongoni alilokuwa nalo alikutwa na kofia nyingine moja pamoja na kitambulisho namba DFF 7001A cha familia ya askari chenye namba 1231 ambacho ni cha mtoto wa askari wa JWTZ MT 65640 Private Gabriel Kihwili wa 501 KJ    kikiwa na picha ya mtoto wake Elia Gabriel.

Uchunguzi bado unaendelea ili kuwapata rafiki zake hao ambao inadhaniwa kuwa huwa wanashirikiana katika kufanya matukio ya kihalifu.