Zanzibar Heroes yawafundisha Kabumbu Tanzania Bara

ZANZIBAR Heroes imedhihirisha kuwa haitanii wala haibahatishi katika michuano ya CECAFA SENIOR CHALLENGE baada ya kuwatandazia kandanda safi na kuwachapa ndugu zao wa Tanzania Bara mabao 2 – 1 katika mchezo wa kundi A uliofanyika katika uwanja wa Kenyatta, County ya Machakos nchini Kenya.

Huo unakuwa ushindi wa pili kwa timu hii chini ya kocha Hemed Moroccco baada ya juzi kuichapa Rwanda 3-1 katika mchezo wake wa kwanza na sasa Zanzibar Heroes wanaongeza matumaini ya kwenda Nusu Fainali.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdul Karim wa Rwanda, aliyesaidiwa na Tigle Belachew wa Ethiopia na Iterve kakunze wa Burundi, Tanzania Bara walikwenda kupumzika wakiwa wanaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Kapteni wao Himid Mao mnamo dakika ya 28.

Kipindi cha pili, Zanzibar Heroes waliongeza kasi ya mashambulizi na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha, lililofungwa na Kassim Suleiman Khamis dakika ya 66 aliyemlamba chenga beki Boniphace Maganga na kuingia ndani ya boksi kabla ya kufumua shuti kutokea pembezoni mwa Uwanja kushoto ambalo lilimpita kipa Aishi Manula.

Wakati Tanzania Bara wakijaribu kutafuta bao la pili, wakajikuta wanafungwa wao kwa shambulizi la kushitukizwa baada ya kiungo mkongwe, Kassim Suleiman ‘Selembe’ kumlamba chenga Maganga na kutia krosi iliyounganishwa nyavuni na Ibrahim Hamad Ahmada dakika ya 78.

Zanzibar Heroes wakapata pigo dakika ya 86 baada ya mfungaji wake wa bao la kusawazisha, Khamis kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Ibrahim Abdallah Hamad.

Tanzania Bara sasa watahitaji ushindi dhidi ya Kenya na Rwanda ili kuangalia uwezekano wa kwenda Nusu Fainali, jambo ni gumu hakika.