Mafunzo wafungua chuo cha ushoni Zanzibar

Akiweka jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha mafunzo ya ushoni Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib, makao makuu ya Vyuo vya Mafunzo Kilimani mjini Zanzibar, amesema Serikali ina azma ya kuendeleza Mapinduzi  kwa kuingiza mapato kwa njia mbalimbali ili kuinua uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla.

Alisema baada ya mapinduzi, Serikali imeamua kujikita katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake kwa kukuza uchumi wa Taifa ili waweze kufaidika na matunda hayo.

Mhe. Salama alisema kazi ya ushoni ina maslahi mazuri kama zilivyo shughuli nyengine, hivyo wanafunzi hawana budi kuchangamkia fursa ya kuwepo chuo hicho na kukitumia kikamilifu kwa ajili ya kujifunza.

Alisema kupata taaluma ya ushoni kuna nafasi kubwa ya kuwapatia ajira za kuajiriwa au kujiajiri, na hivyo kujipatia kipato kitakachowasaidia kuendesha maisha.

“Umuhimu wa jengo hili ni wanafunzi waliofungwa na  wananchi ili waweze kushona sare za askari na zao wenyewe ili fedha za ushoni zisiende nje bali zitumike katika matumizi mengine ya serikali,” alisema Salama.

Aidha alitaka jengo hilo litakapokamilika liwe na utaratibu wa kufanyiwa ukarabati kila baada ya muda  ili kuliimarisha na kuwa kivutio kwa wateja.

Katika risala iliyosomwa na ASP Jaffar Abdullah, imeelezwa kuwa jengo hilo likianza kazi litashonda sare za wanafunzi na maofisa wa vyuo vya mafunzo, pamoja na taasisi mbalimbali.

Hata hivyo, wameitaka serikali kuwaingizia fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ambao awali ulikadiriwa kugharimu shilingi 67,000,000, lakini chuo hicho kimetumia shilingi 21,000,000 kutoka mfukoni mwake.

Naye Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar Ali Abdullah Ali, alisema jengo hilo litakapokamilika litaweza kuchukua zaidi ya wafanyakazi 40 kwa wakati mmoja.

Alisifu juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, kuhakikisha vyuo hivyo vinawekewa mazingira bora ili viweze kuleta tija na kudumisha amani na utulivu uliopo.

“Chuo hicho kitaipunguzia Serikali gharama za kushonesha nguo nje, na fedha zitakazookolewa  zitatumika katika shughuli nyengine za kiuchumi,” alisema.

Ufunguzi wa chuo hicho ni miongoni mwa shamrashamra za kuadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Na Mwashungi Tahir, Maelezo Zanzibar.