Mwenge, Jamhuri taabani, Azam yajiweka pazuri

Timu za soka za Mwenge na Jamhuri zimekubali kupokea vipigo kutoka kwa wageni URA na bingwa mtetezi wa kombe la Mapinduzi Azam FC katika mechi zilizopigwa katika uwanja wa Amaani mapema leo.

Mwenge walikubali kipigo cha goli 1 kwa 0 toka kwa watoza kodi wa Uganda timu ya URA. Goli la URA lilifungwa mnamo dakika ya 27 na Bukota Lubamba hivyo kuifanya URA kufikisha alama 4 huku wakiwa wamebakisha michezo miwili dhidi ya Simba na Azam.

Kwa upande wa timu ya Jamhuri leo imekubali kuchakazwa magoli 4 kwa 0 kutoka kwa Azam FC. Magoli ya Azam yalifungwa na Bernard Arthur mnamo dakika ya 26, Salmin Hoza mnamo dakika ya 47, Yahya Zayd dakika ya 54 na Paul Peter dakika ya 79.

Azam FC imefikisha alama 6 hivyo kuongoza kundi A lenye timu za Simba, URA, Mwenge na Jamhuri huku ikiwa imebakisha mechi mbili za Simba na URA.