Dkt. Mwakyembe aunda kamati ya kusimamia mchezo wa ngumi za kulipwa

TAARIFA KWA UMMA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb) leo tarehe 3 Januari, 2018 amekutana na wadau wa mchezo wa ngumi za kulipwa nchini. Kikao hicho ni mwendelezo wa vikao vya Mhe. Waziri na Wadau hao ili kutatua migogoro iliyodumu kwa muda mrefu katika mchezo huo wa masumbwi ya kulipwa, vikao hivyo vilianza mwishoni mwa mwaka 2017. Katika kikao kilichofanyika leo, Mhe. Waziri aliwaagiza wadau hao kufanya kazi kwa pamoja katika kuunda mfumo mpya utakaolinda maslahi ya mabondia na wahusika wengine wa mchezo wa ngumi za kulipwa na kuliletea Taifa letu heshima kwa kupitia mchezo huo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Ili kupiga hatua, Waziri Mwakyembe ameunda kamati ya watu kumi na moja (11) itakayokusanya maoni ya wadau na kupitia upya katiba ya kuunda Chombo kitakachosimamia mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini. Kamati hiyo imeanza kufanya kazi leo  tarehe  03 Januari, 2018 na itakamilisha kazi yake tarehe 31 Januari, 2018. Kamati itasimamiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na itakuwa na wajumbe wafuatao:-:

 1. Ndg. Emmanueli Salehe         –     Mwenyekiti
 2. Ndg. Joe Enea                      –     Makamu Mwenyekiti
 3. Ndg. Yahya Pori                    –     Katibu
 4. Ndg. Habibu A. Nyogoli         –     Mjumbe
 5. Ndg. Shomari Kimbau           –     Mjumbe
 6. Ndg. Fike Wilson                  –     Mjumbe
 7. Ndg. Anthony Ruta               –     Mjumbe
 8. Dkt. Killaga M.Killaga           –     Mjumbe
 9. Ndg. Ally B. Champion         –     Mjumbe
 10. Ndg. Rashidi Matumla          –     Mjumbe
 11. Ndg. Karama Nyilawila         –    Mjumbe

Aidha, Waziri Mwakyembe ameeleza kwamba katika kipindi cha mpito shughuli za kutoa vibali kwa mapambano ya ndani na kwa mabondia wanaosafiri nje ya nchi zitaendelea kutekelezwa na BMT. “BMT endeleeni kusimamia vibali vya mapambano ya ndani na vibali vya safari za nje ya nchi za mabondia kwa kuzingatia uzalendo, weledi, kanuni na sheria za nchi bila kumwangalia mtu usoni wala kumuonea haya”, amesisitiza Waziri Mwakyembe.

 

Imetolewa na

 

Octavian F. Kimario

Kaimu Mkuu waKitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

03/01/2018