TRA yabuni njia ya kuongeza ukusanyaji wa kodi 2018

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa inatarajia kusajili walipakodi wapya takribani 1000,000  ambao kwa pamoja wanakadiriwa kuwa wataongeza mapato yatokanayo na kodi kwa kiwango cha Sh. Bilioni 1.5 kwa mwaka.

Mfanyakazi wa TRA Bi. Regina Urio akichukua taarifa za mmoja wa wakazi wa Chanika Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam aliyefika katika kituo cha kusajilia walipa kodi wapya zoezi lililoanza jana jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa zoezi la usajili wa wafanyabiashara wadogo zoezi lilionza jana katika Eneo la Chanika Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Kodi za Ndani, Elijah Mwandumbya amesema kuwa kampeni ya kusajili wafanyabiashara wadogo ni endelevu.

“Zoezi hili la usajili wa walipa kodi ni endelevu, lengo letu kama Mamlaka ya Kodi Tanzania ni kuhakikisha tunawasogezea huduma wateja wetu lakini pia tunatimiza wajibu wetu wa kukusanya kodi.” Alisema Mwandumbya.

Aidha Mwandumbya alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo ili waweze kusajiliwa kama walipa kodi na kupatiwa Namba za Utambulisho wa Mlipa kodi (TIN).

Amesema kuwa uhamasishaji wa ulipaji kodi na usajili utaendelea kwa kuweka vituo karibu na wafanyabiashara.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka hiyo Richard Kayombo amewataka wananchi wanaoishi Chanika na maeneo jirani ikiwemo Mvuti kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kujiandikisha  na kusema kuwa zoezi hilo katika Kituo hicho litadumu kwa muda wa siku tano hivyo ni vyema wakatumia fursa hiyo kupata huduma hiyo inayotolewa bure.

“Usajili wa walipa kodi katika eneo hili la Chanika utadumu kwa siku tano, baada ya hapo tutahamia maeneo ya Tabata Segerea na Kisukuru, na kisha zoezi litaendelea Manispaa ya Temeke na baadaye Kinondoni huku tukifungua vituo katika maeneo mbalimbali,” alisema Kayombo.

Aidha Kayombo amesema, Mamlaka hiyo imeamua kuja na kampeni hii  baada ya kutambua kuwa kulikuwa na usumbufu kwa wafanyabiashara kupata TIN namba, kutokana na umbali kutoka wakazi wa eneo hilo hadi Vingunguti.

Pamoja na hayo amewatahadharisha wananchi kutolaghaiwa na matapeli kwani kazi hiyo inafanywa na TRA yenyewe na hakuna wakala aliye pewa kazi hiyo.