Wanawake Pemba wasema sasa basi

WANAWAKE wajasiriamali kisiwani Pemba, wamesema sasa wakati wa kusubiri uamuzi kutoka kwa wanaume, hata kwenye vikao vya harusi, umemalizika na lazima wanawake wenyewe wafanye uamuzi kwa mambo yanayowahusu.

Wamesema ule utamaduni wa zamani kuwa wanaume ndio kila kitu, umepitwa na wakati na kwa karne hii, lazima wanawake wajitokezea na kujibebesha ujemedari wa kufanya uamuzi.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wanawake hao wajasiriamali, walisema utamaduni wa miaka 30 nyuma kuwa waanume ndio kila kitu hasa kwenye uamuzi, sasa haupo tena.

Mwenyekiti wa ushirika wa upandaji migomba ‘tumeamua ‘shehia ya Kiuyu kigongoni wilaya ya Wete Pemba, Fatma Said Juma, alisema sasa wanawake lazima wathubutu kuendesha vikao na kutoa uamuzi.

Alisema haipendezi na wala haingii akili, kuona wanawake wanashindwa kufanya vikao mbali mbali vikiwemo vya harusi, uamuzi wa kumsomesha mtoto, vikao vya asasi vya kiarai pasi na kuwepo wanaume.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa, sasa wanawake wameshaelimika na kupata ujasiri kwa kufanya shughuli zao mbali mbali za maendeleo, hivyo wasishindwe na kuendesha vikao na mikutano yao.

“Inawezekana wazazi na walezi wetu, sisi wanawake walitunyima haki yetu ya kushiriki na kushirikishwa kwenye vikao mbali mbali, kwa dhana kwamba hatuwezi, lakini sio sahihi’’,alilamika.

Kwa upande wake Mwemyekiti wa Jumuia ya Kuhifadhi Mazingira Vitongoji VECA wilaya ya Chakechake Sifuni Ali Haji, alisema wanawame wanauwezo mkubwa na kupelekea maendeleo makubwa.

“Mimi ni mwenyekiti wa VECA mbona tumeshapata miradi miengi, ingawa kuwa kushirikiana na wenzangu, lakini wenyewe tumekuwa watundu wa kuendesha vikao vyetu.

Alieleza kuwa, uwezo waliojaaliwa na Muumba wa kufanya kazi na kutoa uamuzi, laiti kama hata hao wazazi waliopita wengewashirikisha vya kutosha, leo hii kusingekuwa na wanamke anaelilia kuporwa haki yake.

Nae mwanaharakati wa maendeleo ya wanawake kisiwani Pemba Nassra Salum, alisema baada ya wanawake kujitumbukiza kwenye ujasiriamali na kujipatia maendeleao, hawana sababu ya kushindwa ya kuendesha mambo mengine.

Alifahamisha kuwa, wanawake wamekuwa na mchango mkubwa ndani ya familia na hata serikali kuu, hivyo lazima nafasi yao hiyo, wasiiache na kuona kuwa wanaume wanaweza kila kitu.

“Yapo mambo ya asili yake lazima wanaume wawe juu, mfano wa mirathi, lakini hakuna ulazima wala sheria kuwa, vikao na mikutano mbali mbali kwamba wanaume ndio wawe wasemaji wa kuu na waamuzi’’,alifafanua.

Nae Maulid Saleh Hamad wa Kiuyu Jimbo la Kojani, alisema wapo wanawake waanaoendesha familia zao, kutokana na kuamua kujiingiza kwenye ujasiriamali, na kupata mafanikio.

“Sasa wanawake lazima tuachane na utamaduni wa zamani kwamba kila kikao na kila jambo eti wasubiriwe wanaume, na kama hawakuja kivunjike, hili sasa sio sahihi”,alifafanua.

Hata hivyo hivyo Mwenyekiti wa ushirika wa wasusi wa mikoba na utengenezaji sabuni wa “subira njema” uliopo Changaweni Mkoani, Amina Said  alieleza kuwa, usawa kwenye kujiinua kiuchumi, uko sawa baina ya jinsia mbili.

Hata hivyo Mratibu wa TAMWA Zanzibar Mzuri Issa Ali, aliwataka wanawake wasikubali kutafutiwa haki na uamuzi na wanaume, bali sasa wasimame wenyewe.

“Sisi tumeshwapa taaluma ya kujielewa na kujiendeleza kiuchumi, sasa kama wameona kuwa wanauwezo wa kujiendeleza, ndio tunakotaka kwenda huko, kila mmoja asimame mwenyewe’’,alifafanua.

Kwa upande wake Hassan Haji Khamis mkaazi wa Machomane Chakechake, alisema wanawake wakiendelea kupewa elimu na nyenzo za kujiletea maendeleo, wanaweza kujihudumia wenyewe.

“Inawezekana hapo zamani wanawake walikuwa hawajapata taaluma na kujielewa kuwa wanahaki sawa kwenye kutoa uamuzi au kuitisha vikao, pasi na kusubiri wanaume’’,alifafanua.

Hata hivyo mwanasheria Mohamed Hassan Ali, wakati akiwasilisha mada kwa vikundi vya wanawake wa mkoa wa kaskazini Pemba, alisema maendeleo hayamsubiri mwanamke eti mpaka ashirikishwe kwenye uamuzi na wanaume.

“Mwanamke na mwanamme wako sawa, wote wanaweza kuwa viongozi na kuongoza vikao, na kisha kufanya uamuzi pasi mmoja kumsubiri mwenzake’’,alifafanua.

Katika miaka ya hivi karibuni kundi la wanawake hapa Tanzania na visiwani, wamekuwa wakijitokeza kwenye shughuli mbali mbali za kujieletea maendeleo, ambapo zaidi ya asilimia 35 ya wanawake ni wafanyabiashara ndogo ndogo.

Na Biabu Zume, Pemba