Mc Pilipili awaanika wavaa utupu baada ya Gigy Money kuitwa BASATA

Baada ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kumuita msanii wa Bongo Fleva Gigy Money na Mwanamitindo Sanchoka kwa mahojiano maalumu kuhusu kazi zao ambazo zinaonekana zipo kinyume na maadili hususani kwenye mavazi wanayovaa wakiwa nusu uchi, Hatimaye Mchekeshaji maarufu nchini Tanzania, MC Pilipili ameipongeza Serikali kwa hatua hiyo na kuishauri iendelee kuwasaka wengine wanaofanya hivyo.

MC Pilipili amesema amepokea taarifa hizo kwa mikono miwili ingawaje amesema kuna watu wengi mitandaoni wanafanya makosa kama hayo ya kuvaa nguo fupi au kuonesha maungo yao kwenye mitandao.

“Hiyo hatua mimi nimeipenda kwanza imeturudisha kwenye Maadili..Unajua hapa Bongo mtu anaweza akawa maarufu kwa kuposti maumbo yake tuu mtandaoni hii ni kinyume cha maadili,“amesema MC Pilipili na kuongeza kuwa “Nilipatwa na maswali juzi Sancho ameitwa, Gigy Money kaitwa lakini pia kuna msanii mwingine alikuwa maarufu kwa kuposti picha kama hizo amejichora mitatuu anaitwa Agness, mwingine anaitwa Kim Sasha lakini wakati huo namuona Idris naye amevaa chupi hivi ile haihamasishi au naye aitwe?“amesema MC Pilipili.

MC Pilipili amesema kuwa video nyingi za wasanii wa Bongo Fleva hazizingatii maadili ya Mtanzania kwani wahusika kwenye video hizo hususani Wanawake huwa wanakuwa nusu utupu.

MC Pilipili amesema kwa upande wake anavutiwa na Alikiba kupitia wimbo wake wa Seduce Me kuwa ni wimbo bora uliozingatia maadili ya kitanzania na bado video imetazamwa na mamilioni ya watu mtandaoni licha ya kukosekana kwa wavaa utupu kama wanavyofanya wengine.