mafuriko yasababisha kufungwa kwa shule Tanzania

Serikali imefunga shule tatu kwa muda katika Wilaya ya Chemba baada ya kujaa maji yanayotokana na mvua zinazoendelea mchini.

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amesema leo Jumatano kuwa shule zilizofungwa ni shule za msingi Oliborot na Kaloleni na Shule ya Sekondari ya Mrijo chini.

“Hizi shule zimezingirwa na maji tumeamua kuzifunga hadi hapo hali itakaporejea kuwa nzuri. Kwa Shule ya Sekondari ya Mrijo chini watu wanaoishi maeneo hayo hawawezi kutoka kwenda sehemu nyingine,” amesema.

Amesema kufuatia wakazi wa eneo hilo la sekondari kushindwa kutoka kwenda sehemu nyingine Jeshi la Zimamoto wamefika wakiwa na vifaa ili kuwaokoa na kuwapeleka katika eneo salama.

Amesema kaya zaidi ya 1,000 kutoka katika vijiji vitatu vilivyokumbwa na mafuriko hayo wamepatiwa hifadhi katika shule ya Mrijo Chini ambapo wanaendelea kupatiwa huduma za lazima ikiwemo chakula.

“Tumetenga madarasa  mawili ambayo yanatumika kwa watu walioondolewa na wengine wamehifadhiwa kwa ndugu na jamaa zao,” amesema.

Amesema kamati za maafa za wilaya na mkoa zinaendelea na vikao vyao kuona namna ya kushughulikia janga hilo.