Wavaa nguo zisizonaheshima hatimae wafikishwa Mahakamani

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limetangaza kufanya msako mkali mwaka huu, kwa watu wanaovaa nguo zisizo na heshima, kulingana na maadili ya Tanzania na kuwafikisha mahakamani.

Akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, wakati akitoa taarifa ya hali ya usalama kwa mwaka 2017, alisema hivi sasa kuna wimbi la mavazi yasio sahihi na hayaendani na utamaduni wa Tanzania.

Amesema kutokana na kukithiri kwa hali hiyo wameamua kuendesha msako ili kuwakamata wahusika na kuwafikisha mahakamani wakiwa na nguo zao walizokutwa nazo ili ndugu na jamaa zao wawaone.

Mkumbo amegusia pia matukio ya kubaka na kulawiti yameongezeka, tofauti na matukio mengine yamepungua sababu ya jitihada za Jeshi hilo kutoa elimu kwa wananchi.

Amesema matukio ya kubaka kwa mwaka 2016 yalikuwa 144 ambapo mwaka 2017 yameongezeka hadi kufikia 149, huku makosa ya kulawiti yakiongezeka toka 58 mwaka 2016 hadi 62 mwaka 2017.

Amesema sababu kubwa ya kuongezeka kwa makosa hayo ni sababu ya mila potofu, imani za waganga wa kienyeji na ukosefu wa elimu. Aidha alisema ni vema kila Mtanzania akafahamu makosa hayo hayafai na yana adhabu kubwa ya kifungo cha miaka 30 au maisha jela.