Amani ndio kichocheo cha wawekezaji Zanzibar – Dkt. Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein  amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kudumisha amani  iliyopo kwani ndio chachu ya  kuvutia wawekezaji  kuja kuekeza miradi  yao ya maendeleo Zanzibar.

Akizungumza katika uwekaji wa jiwe la msingi la  mji wa kisasa fumba ‘fumba town development’ amesema wawekezaji wamekuwa wakishajihika kuekeza nchini na wageni mbalimbali kuja kutembea kutokana na nchi kuwa ya amani na utulivu.

Amesema Serikali itaendelea  kuwashajihisha  wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kuwekeza Zanzibar kwani bado kuna maeneo mengi yanahitaji kuwekezwa yakiwemo kwahani, kijangwani, kwalimsha, kariakoo,  Mkokotoni, chwaka na tunguu ambayo wanaweza kuekeza kwa ujenzi wa nyumba za kisasa ili kuubadilisha mji wa Zanzibar.

Aidha amesema  kufanya hivyo kutasaidia kwa  kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira linalowakabili vijana wengi nchini hasa waliomaliza elimu ya juu na kuwataka  vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na wawekezaji hao pindi zinapotokea ili kujikwamua kiuchumi.

Akizungumzia suala la Ardhi amesema  kuwa ardhi yote Zanzibar ni mali ya serikali na kuwataka wananchi kuwacha tabia ya kugombania ardhia kwani hupelekea migogoro isiyo na tija ambayo inarudisha nyuma maendeleo.

Amesema Serikali itafanya kila njia katika kubana matumizi bora ya ardhi  katika harakati za ujenzi  ili kuwawezasha  wananchi  kupata makaazi bora ya kuishi.

Kwaupande wake Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa fumba Sebastian Dezot amesema lengo la mradi wao huo ni kurahisisha upatikanaji wa makaazi bora ya kuishi wananchi wa Zanzibar pamoja na kuwainua kiuchumi  hasa vijana kwa kuwapatia ajira kupitia mradi huo wa ujenzi.

Amesema Jumla ya Dolla  Million 25 zilitumika katika mradi wa ujenzi wa nyumba hizo  na matarajio yao ni kuendelea kujenga zaidi  nyumba ikiwemo horofa na za chini.

Nae Waziri wa fedha na mipango Dr.Khalid Salum Mohammed amesema Zanzibar imeweza kupiga hatua za maendeleo katika ukusanyaji wa mapato kutoka sehemu mbalimbali za uwekezaji na sasa jumla ya miradi 42 imeweza kuwekezwa nchini.

Amina Omar.