BAVICHA wamjia juu kaimu katibu mkuu UVCCM kisa Tundu Lissu

Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) Julius Mwita amesema kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka huenda ana matatizo ya akili.

Mwita amesema hayo leo Januari 11, 2018 katika Mkutano na waandishi wa habari wakati akijibu tuhuma alizotoa kiongozi huyo wa UVCCM dhidi ya Tundu Lissu ambapo alisema kuwa Tundu Lissu ni muongo na hapaswi kuaminiwa kwani anatafuta tu umaarufu.

Kufuatia kauli hiyo ya Shaka ndipo hapo viongozi wa Baraza la Vijana wa Chadema walipoamua kusema “Tumetafakari kauli ya Shaka kwa kina na tumejaribu kufikiri kama Shaka ana akili timamu au ni kichaa? Kwa sababu kama chama chake chenyewe wamekiri pamoja na Serikali hawawezi kuzungumza suala la Lissu kwa sababu ni mgonjwa na yupo hospitali, Shaka anapata wapi ujasiri wa kuja kuzungumza mambo yanayomuhusu Tundu Lissu tena kwa kuzungumza mambo ya uongo na ushahidi usio na tija yoyote na anawadanganya Watanzania kuwa katika nchi hii Lissu siyo wa kwanza kupigwa risasi” alisema Mwita

Ameongeza Mwita kuwa“Tulitegemea umoja wa vijana wa chama ambacho kinaendesha Serikali watoke wawaambie Watanzania kwamba tunakitaka chama chetu yaani kiiagize Serikali kutibu mgonjwa ambaye yupo hospitali na ameshambuliwa katika majukumu yake ya Ubunge lakini Shaka anatoka kupotosha kwa maneno ya kejeli na ya kihuni. Lakini tumkumbushe Shaka, Amani Abed Karume hakuuawa kwa sababu za kisiasa na wala hajawahi kuwa mpinzani, wala hajawahi kuwa mkosoaji wa Serikali iliyopo madarakani kwa wakati huo useme kwamba alishambuliwa kwa sababu ya ukosoaji wake bali kulikuwa na sababu zingine tofauti zilizopelekea Karume kushambuliwa” 

Siku kadhaa zilizopita Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alifunguka na kuishtumu Serikali ya awamu ya tano kuhusika katika kushambuliwa kwake baada ya kali hiyo Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka naye alimjibu Tundu Lissu na kusema kuwa mwanasiasa huyo ni muongo na anatafuta umaarufu.