Mhe. Makonda atoa miezi 4 kwa Wafanyabiashara soko la Urafiki

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda amewapa muda wa miezi 4 wafanyabiashara wadogo wadogo wa Soko la Urafiki linalojulikana kama Mahakama ya Ndizi kuhama katika eneo hilo kutekeleza agizo la Mahakama kwa kuwa eneo hilo ni mali ya kiwanda cha urafiki

Makonda amesema hayo leo na kudai kuwa wafanyabiashara hao hawawezi kuhamishwa kama ilivyokuwa awali bali wanatakiwa kuhama baada ya miezi minee kupita na kusema wakati huo Serikali itakuwa imeshawaandalia eneo maalum la kwenda ili kuepukana na matatizo kama hayo tena.

“Mtafanya biashara kwenye hili eneo kwa muda wa miezi minne hamtaondolewa leo wala kesho kama ilivyokuwa imepangwa bali tumeongeza siku 120 lakini pia nimemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo tayari kuna eneo limepatikana, tunataka tukamilishe utaratibu wa uhalali wa lile eneo ili watu wakienda pale wasipate matatizo kama haya yanayojitokeza ya kufukuzana fukuzana” alisisitiza Makonda

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa katika eneo ambalo watapewa litakuwa limeboreshwa zaidi ili wafanyabiashara hao waweze kupata wateja wa kila aina kwa kudai kuwa walipo sasa wanawakosa baadhi ya wateja kutokana na miundombinu ya soko hilo kutokuwa rafiki kwa baadhi ya watu.