Serikali ya Cuba imetiliana Saini na SMZ kwa Usomeshwaji wa Madaktari 15

Serikali ya Jamuhuri ya Cuba  imetiliana Saini Mkataba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Usomeshwaji wa Madaktari  Wazalendo 15 wa Zanzibar  Nchini Cuba katika Fani ya Shahada ya Uzamili ya Udaktari.

Madaktari hao 15 ambao Wanane wa Mwanzo  wataanza Mafunzo yao Mwezi ujao wakifuatiwa na wengine  7 wa awamu ya Pili ni Miongoni mwa Wanafunzi waliomaliza masomo yao kupitia mpango wa masomo ulioasisiwa kati ya Serikali ya Cuba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Saini ya Mkataba huo kwa Serikali ya Cuba imewekwa na Balozi wa Nchi hiyo Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernades na kwa upande wa Zanzibar Saini ikatiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar  Bibi Halima Maulid Salum.

Hafla hiyo fupi ya Kihistoria imeshuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyejumuika pamoja na baadhi ya Mawaziri wa Wizara husika, Watendaji wa Wizara hizo na kufanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernades alisema  Cuba bado inaendelea kutafakari maeneo mapya  zaidi inayoweza kushirikiana na Zanzibar katika kuendelea kupiga hatua kubwa zaidi za Kiuchumi na Maendeleo.

Balozi Lucas alisema suala la kuwafanya Wananchi wa Visiwa  vya Unguja na Pemba wanakuwa katika ustawi ulio bora zaidi wa afya na kipato  limepewa kipaumbele na Serikali ya Cuba kuliko jambo jengine lolote la ushirikiano wa pande hizo mbili.

Balozi wa Cuba Nchini Tanzania alielezea faraja yake kutokana na ukarimu anaoushuhudia wa Watu wa Zanzibar kwa wageni jambo ambalo limempa nguvu na ari zaidi ya kuona jinsi gani anaweza kuitumia fani yake ya Diplomasia katika kudumisha udugu wa pande hizo mbili.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  alisema mkataba huo  wa Usomeshwaji wa Madaktari  Wazalendo wa Zanzibar  Nchini Cuba umejenga historia  mpya ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Cuba katika  Sekta ya Afya kuelekea mfumo wa kisasa wa Sayansi na Teknolojia Ulimwenguni.

Balozi Seif aliishukuru na kuipongeza Jamuhuri ya Cuba kupitia Balozi wake Nchini Tanzania kwa ukarimu wake wa kupungua kima cha malipo kwa Wanafunzi hao wa Fani ya Udaktari katika ngazi ya Shahada ya Uzamili ya Udaktari.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Balozi Lucas Domingo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanmzania zitaendelea kuupa ushirikiana ubalozi huo ili uendelee kutekeleza vyema majukumu yake ya Kidiplomasia.

Mapema Waziri wa Afya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo  alisema uhusiano wa Sekta ya Afya kati ya Zanzibar na Cuba  umeanza kupata baraka zaidi kufuatia Ziara ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Zanzibar aliyoifanya Nchini Cuba  Mnamo Mwaka 2008.

Mh. Mahmoud  alisema baraka hizo zimewezesha kuanzishwa kwa Chuo cha Madaktari Zanzibar ambacho tayari kimeshazalisha Madaktari Wazalendo 50 waliosomeshwa chini ya Wahadhiri na Wataalamu kutoka Cuba kupitia mpango wa masomo ulioasisiwa kati ya Zanzibar na Cuba.

Waziri Mahmoud alifahamisha kwamba mafunzo hayo yamekuwa yakiendelea kwa makundi mengine ya Udaktari  kila Mwaka ambapo mfumo uliopo hivi sasa  kwa mafunzo hayo umejumuishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar {SUZA}.

Alisema ushirikiano wa Kidiplomasia kati ya Jamuhuri ya Cuba na Zanzibar umeasisiwa Mnamo Mwaka 1964, Cuba ikiwa ni miongoni mwa Mataifa Matano ya Kwanza  yaliyoitambua  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  mara baada ya Mapinduzi  Matukufu ya Zanzibar  ya Mwaka 1964.

Jamuhuri ya Cuba kupitia Balozi wake Nchini Tanzania katika Mkataba huo uliowekwa saini imeridhia kupungua kima cha malipo kwa kila Mwanafunzi katika Kundi hilo la Madaktari 15 Wazalendo wa Zanzibar  katika ngazi ya Shahada ya Uzamili ya Udaktari.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

13/1/2018.