Mzee Majuto anena mazito baada ya kutembelewa na Rais Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli  leo Januari 31, 2018 amemtembelea muigizaji mkongwe, Mzee Majuto katika hospitali ya Tumaini jijini Dar es salaam anapopatiwa matibabu.

Akizungumza mara baada ya kutembelewa na Rais, Mzee Majuto amefunguka na kudai yeye ndio mtu wa kwanza kutabiri ujio wa Rais Magufuli katika kuongoza nchi ya Tanzania huku akisisitiza kwamba anajisikia faraja kuona ana misimamo iliyokuwa imara.
“Mimi ndiyo mtu wa kwanza kumtabiri kwamba akiwa Rais itakuwa shughuli. Nilishukuru sana kuchaguliwa huyu bwana, tumepata Rais sio masihara watu wote sasa hivi wana adabu zao wanajua nini maana ya kazi”, alisema Majuto.
Pamoja na hayo, Mzee Majuto aliendelea kwa kusema ;“sisi wazee tunafarijika sasa hivi, viwanda kila kona vimetapakaa na leo amekuja kutembea hospitalini hapa sijui kama wengine hawajajikojolea huko kwa uoga maana hataki masihara. Hii ndio raha ya kupata viongozi wenye msimamo”.
Mzee Majuto awali alikuwa akitibiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili.