Raia wa Argentina akutwa amekufa katika hoteli ya Tembo Shangani Unguja.

Edward Maselo mwenye miaka 48, Raia wa Argentina ameripotiwa kufariki dunia katika hoteli ya Tembo Huko Shangani Mjini Unguja.

Akithibitisha kufariki kwa mtalii huyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Hassan Nasir Ali amesema mnamo February, 2 mwaka huu majira ya saa 11:56 Jioni walipokea taarifa ya kifo cha mtalii huyo ambapo hadi sasa hawajabaini chanzo chake na hakuna wanaemtuhumu kuhusika na kifo hicho.

Kamanda Nasir amesema kwa mujibu wa wahudumu hotelini hapo wamesema marehemu kabla ya kifo chake alikuwa chumbani kwake ambapo walimgongea majira ya saa 4 asubuhi wakimtaka atoke kupata chai ya asubuhi ambapo aliwajibu wamuache amepumzika.

Hadi kufika jioni alikuwa kimya ndipo wakapatwa na hofu, walipofungua mlango wa chumba chake walimkuta chini sakafuni akiwa teari ameshafariki dunia.

Aidha kamanda Nasir amesema uchunguzi wa kidaktari umefanyika na teari mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa  ubalozi wa nchi yake uliopo hapa nchini kwa ajili ya taratibu nyengine za mazishi.

Hatahivyo Kamanda amebainisha kuwa wao kama Polisi wataendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo kilichopelekea kifo cha mtalii huyo.