Diamond na Mobeto mambo safi kesi ya malezi ya mtoto

Msanii wa Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz amesema kuwa mazungumzo katika kesi ya malezi ya mtoto wake na Hamisa Mobeto yaliyofanyika leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kitengo cha watoto yamemalizika vizuri kwa wao kufikia maamuzi kuhusu namna ya kumlea mtoto wao.

Diamond amesema yeye na Mobeto hawana shida yoyote, ila kuna watu wa pembeni waliokuwa wakizungumza maneno na kumchochea Mobeto.

“Ikitokea kuna mtafaruku baina ya mtoto, kila mtu anakuwa na mawazo yake, kwa hiyo ni lazima kumjenga mtoto na kuhakikisha kuwa mtoto anajengwa na kulelewa  katika malezi bora,” alisema Diamond.

Diamond hakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha ambacho wameandikishana kutoa kwa ajili ya malezi ya mtoto.

“Mtoto ana mahitaji mengi wakati mwingine mtoto wako unaweza kumpa hata Sh100 milioni. Huwezi kusema siwezi kumpa kwa sababu niliandikisha nitampa Sh100,000. Tumeweka mazingira mazuri ya kiasi kitakachomfanya akue katika malezi bora,” amesema.

Aidha, msanii huyo amesema kwamba, kupitia mahakama ameweza kujifunza mambo mengi kuhusu malezi na kwamba wakati wowote atakapohitajika atakwenda.

Amesema atahakikisha mtoto huyo anakuwa katika mazingira mazuri anamsomesha kadri ya uwezo wake utakavyoruhusu kwa maelezo kuwa maisha ni kupanda na kushuka.