Tanzia: Mratibu wa kampeni jimbo la kinondoni Chadema afariki dunia.

Mwanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Richard Tambwe Hizza amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Februari 8, 2018 akiwa nyumbani kwake.

Mwili wake umepelekwa Hospitali ya Temeke Dar Es Salaam asubuhi hii. Hadi jana saa tano usiku alikuwa kwenye Kikao cha CHADEMA.

Kwa mujibu wa mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Salum Mwalimu aliiambia East Africa Radio kuwa “Ni kweli Tambwe Hizza amefariki nami nimetumiwa ujumbe mfupi mara nilipofika hapa Radio, kama kiongozi wa chama, hivyo naomba tupewe muda kidogo ili tuweze kufahamu zaidi chanzo cha kifo chake maana imekuwa ghafla sana kutokana mpaka jana usiku saa 5 nilikuwa nae”, amesema Mwalimu.

Marehemu Tambwe Hizza amefariki akiwa ni mmoja wa waratibu wa kampeni za chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) katika jimbo la Kinondoni ambapo Jana alishiriki kampeni za kumnadi Salum Mwalimu Tandale mapema jioni kabla ya Vikao vya chama.

Hizza anafahamika sana kwa siasa zake akiwa CUF, Baadae alihamia CCM na kuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda wa CCM na 2015 aliamua kuondoka CCM na kuhamia CHADEMA. Mwaka 2014 alisema angegombania Urais kupitia chama cha mapinduzi kwani uwezo, akili, elimu na afya ya kumuwezesha kuwa Rais wa tano wa Tanzania anao.