Dkt. Mabodi akoshwa na miradi ya TASAF

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar (CCM), Mhe:Dk Abdalla Juma Mabodi, amesema mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania (TASAF), kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini Zanzibar, umefanikiwa kutekeleza ilani ya CCM kwa asilimia 98% katika miradi yake mbali mbali.

Mabodi alisema miradi mingi ya Tasaf imetekelezwa kwa hali ya juu, jambo ambalo limeweza kuzisaidia baadhi ya taasisi za serikali, kupitia miradi hiyo na kunyanyua hali za maisha ya wananchi masikini.

Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, aliyaeleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Kisiwani Pemba, mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea miradi mbali mbali, inayotekelezwa na mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania (TASAF), kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini kwa upande wa Zanzibar.

Alisema mafanikio makubwa yamepatikana kupitia mpango huo, kwani miradi mbali mbali imeweza kuwasaidia wananchi na kuwainua katika kipato chao cha kimaisha.

“Tizameni Junguni watoto wetu ndugu zetu, wanasoma bila ya matatizo yoyote, kupitia mpango huu wa Tasaf, kwenye Ilani tumesema lazima watoto wote wapate elimu ya maandalizi, skuli imejengwa na wanafunzi kutoka maeneo mbali mbali wanasoma hapa”alisema.

Alisema mpango huo umeweza kupunguza hata utoro wa wanafunzi maskulini, hilo ni jambo la kuipongeza serikali kwa hatua iliyofikiwa.

Akizungumzia suala la mabadiliko ya Tabia nchi, alisema sera ya CCM ni kutunza mazingira, hivyo kuwepo kwa matuta ya kuzuwia maji chumvi kwa wanakaya masikini, moja ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa vitendo.

“Suala la Mazingira linashuhulikiwa na Serikali zetu mbili, SMT na SMZ, nijambo zuri mazingira yetu kuyaweka sawa kwa hali yoyote ile”alisema.

Aidha aliwapongeza wananchi kwa kutokuingiza siasa katika masuala ya Maendeleo, hivyo aliwataka kuweka pembeni siasa zao na wakati wa siasa umepita, kilichobakia kujenga Zanzibar na kulinda amani na utulivu iliyopo nchini.

Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, aliwataka viongozi wa Chama na Serikali kufika kwa wananchi wa chini, kujuwa matatizo yanayowakabili na sio kukaa maofisini tu.

“Tulipohitaji kura ili CCM tuirudishe tena madarakani, tulifika huku kwa wananchi hawa hawa kwa miguu, tena usiku wala hatukujali umbali au vipi, iweje leo tuwazarau tutaendelea kuwathamini na kuwatunza nyinyi ni muhimu kwetu”alisema.

Akizungumzia ukarabati wa njia ya kinyikani hadi Piki yenye urefu wa Kilomita 3, aliwapongeza wanakaya masikini kwa kubunjia mpango huo, ambapo mikakati ya Wizara ni kuitengeneza barabara hiyo.

“Wanakaya wa kinyikani wamefanya jambo kubwa sana, njia hii itaweza kurahisisha shuhuli za usafiri, kilimo, hata kufuata huduma za kijamii sasa ni rahisi kwao”alisema.

Mwakilishi wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Pemba, Hashim Juma Mohamed alisema barabara hiyo imo katika mpango wao wa mwaka huu wa kuitengeneza.

Ujenzi wa njia hiyo umeambatana na utengenezaji wa kalavati la kupitishia maji, lililogharimu Milioni 6,027,500/=, nguvu kazi za wananchi ni 2,587,500/= huku Tasaf 3,440,000/=.