Polisi wapambamoto kuondoa uhalifu Watatu watiwa mbaroni Zanzibar

Zaidi ya shilingi Milioni tano zimekusanywa kutokana na makosa mbalimbali ya usalama Barabarani yaliyojitokeza   katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kwa wiki iliyoishia Februari 11, 2018.

Akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na Matukio ya wiki ya Mkoa wa Mjini Magharib Unguja Kamanda wa Polisi Mkoa huo Hassan Nassir Ali, amesema makosa 247 ya usalama barabarani yamejitokeza ambapo makosa 182  yalifikishwa mahakamani na kutozwa fedha hizo taslim kama adhabu na makosa yaliyobakia yanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

Amesema katika kukabilia na wavunjifu wa sheria za Barabarani Jeshi hilo linaendelea na msako ili kuwakamata madereva wanaovunja sheria na kuhatarisha maisha ya wananchi hususani wanaotembea kwa miguu.

Akizungumzia suala la utumiaji na Usambazaji wa dawa za kulevya kamanda Nassir amesema wanawashikilia watu watatu akiwemo Rajabu Ramadhani Sleimani (24) mkaazi wa Bububu akiwa na kete 7 za dawa za kulevya, Juma Abdi Juma (35) akiwa na nyongo 78 zinazosadikiwa kuwa ni bangi na Imani Kasim Haji (19) akiwa na kete 109 zinazosadikiwa ni Dawa za kulevya.

Kamanda Nassir ametoa wito kwa taasisi na wananchi kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano na Jeshi la Polisi katika kukomesha matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana.