Picha: Mhe. Samia akitoa mjumuisho wa ziara yake Iringa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa mkoa wa Iringa kushirikiana ili kuweza kuwasaidia wananchi wa mkoa huo.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa kutoa mjumuisho wa ziara yake ya kuhamasisha shughuli za maendeleo mkoani Iringa.

Makamu wa Rais alitembelea wilaya ya Iringa, Kilolo na Mufindi ambako kote alishiriki shughuli za kimaendeleo ikiwemo kuzindua Vituo vya Afya Kising’a wilayani Iringa, Jengo la Utawala na Madarasa katika Shule ya Sekondari Kilolo,

Pia aliweka jiwe la msingi katika Ujenzi wa Maabara na Madarasa katika shule ya sekondari Mgololo na kuweka jiwe la Msingi katika upanuzi wa Kituo cha Afya cha Ihongole kilichopo Mafinga.

Makamu wa Rais pamoja na kutembelea miradi hiyo ya kimaendeleo pia alitembelea Kiwanda cha Ivori kinachotengeneza pipi na Chocolate na alitembelea kampuni ya GBRI inayoshughulika na uzalishaji na uuzaji wa bidhaa za mbogamboga.

Katika ziara hiyo Makamu wa Rais aliwapongeza wananchi wa mkoa wa Iringa kwa mapokezi mazuri waliompa kipindi chote cha ziara yake.

Makamu wa Rais alisisitiza juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na utunzaji mazingira, Aidha Makamu wa Rais aliwataka viongozi wa mkoa huo kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya mazingira na elimu juu ya ugonjwa hatari wa Ukimwi ambao unaonekana kuenea kwa kasi mkoani humo.

Makamu wa Rais aliwataka viongozi kutoa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya Jamii.

Makamu wa Rais alitoa rai kwa Viongozi na Wananchi kuunga mkono mradi wa kuendeleza utalii ukanda wa kusini mwa Tanzania (REGROW) aliouzindua jana kwani pamoja na kufungua fursa mkoani humo lakini pia utasaidia katika kutunza mazingira.

Mwisho Makamu wa Rais aliwaahidi kubeba changamoto zote kubwa zikiwemo za barabara na huduma za afya ambazo bado ni kilio kikubwa mkoani humo.