SMZ yajadili kuwaangalia upya waendesha bodaboda

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Serikali ya mapinduzi kuifanyia marekebisho sheria ya vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri  kwa wananchi ili kuwapa fursa waendesha bodaboda kuingia katika sheria hiyo itakayo waruhusu kupakia abiria kihalali.

Akiuliza swali la nyongeza Mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele Suleiman Shihata juu ya uwepo wa  waendesha bodaboda  na kuweza kufahamika kisheria amesema “Serikali haioni haja  kwa waendesha bodaboda kupewa usajili rasmi ambao utatambulisha uwepo wao juu ya ufanyaji wa kazi zao?”.

Akijibu swala hilo Naibu Waziri  Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mohammed Ahmada amesema kwa mujibu wa sheria namba 7 ya mwaka 2003  kifungu cha 82 Bodaboda haziruhusiwi kubeba abiria  lakini watafanya utaratibu wa kukaa na wadau kuzungumza na kulijadili suala hilo na mwishowe kulifikisha Serikalini.

Kwaupande wao baadhi ya Waendesha bodaboda wakizungumza na Zanzibar24  wametoa maoni yao  juu ya hoja hiyo na kuiomba Serikali ya mapinduzi kukubali kuifanyia marekebisho sheria  hiyo  kwani  bodaboda  imeweza kutoa ajira kwa vijana wengi na kurahisisha  huduma za usafiri kwa wananchi.