Wananchi washiriki kutimiza dhana ya utawala bora Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa , Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri amewataka  wananchi  kuchangamkia fursa za uongozi  katika mabaraza  ya wadi, kamati za shehia na katika ngazi mbalimbali za uongozi kwenye serikali za mitaa kwa lengo la kutekeleza kwa vitendo ile dhana ya utawala bora na ushirikishwaji wa wananchi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Februari 13, 2018 katika ukumbi wa baraza la wawakilishi la zamani Kikwajuni mjini Unguja Mhe. Haji amesema, wakati umefika Wananchi wakubali kushiriki katika nafasi za uongozi zilizo  katika ngazi za shehia  au wadi ili kusaidia kuibua  changamoto zinazowakabili wananchi na serikali kuweza kuzifanyia kazi kwa misingi ya sheria

Mhe. Haji amesema dhana ya serikali ni uundwaji wa mabaraza ya wadi na kamati za mashauriano ya shehia  kwa mujibu wa  vifungu vya sheria  namba 42 na 47 ya  sheria  ya mamlaka ya  serikali za mitaa ya namba 7  ya mwaka 2014 kwa lengo la kutoa madaraka kwa wananchi ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini Mkuza I, II ,III pamoja na ile dhana ya utawala bora kutekelezeka kwa vitendo.

Hata hivyo amesema kuanzishwa kwa mabaraza hayo katika  wadi na shehia lengo ni kutoa huduma bora ambazo ni endelevu kwa wananchi na kuzingatia misingi ya utawala bora pamoja na  kuwepo kwa ushirikishwaji wa wananchi katika kubuni, kuibua, kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo katika shehia zao, kwa kuzingatia uwajibikaji na uwazi.

Akizungumzia utekelezaji wa hatua hiyo ya  ugatuzi wa madaraka wameanza kutoa taalumu  ya dhana nzima  kwa madiwani na sheha kwa pande zote Unguja na Pemba ambayo yaweza kuisaidia serikali katika utekelezwaji wa kazi na majukumu ya wananchi.

Amina Omar