Jeshi la polisi lawashikilia watu watatu akiwemo mwanafunzi wachuo wakiwa na nyara za serikali

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya llimewakamata watu watatu akiwamo anayedaiwa kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) tawi la Mbeya wakiwa na nyara za Serikali ambazo ni vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh33 milioni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga ametoa taarifa za jeshi hilo kuwakamata watu hao ambao wote ni wakazi wa Jiji la Mbeya.

Kamanda Mpinga amesema kwamba polisi wakiwa doria Februari 5 mwaka huu eneo la Mwanjelwa jijini hapa walifanikiwa kuwanasa watuhumiwa hao wakiwa na nyara hizo ndani ya gari lao.

“Baada ya kukamatwa na kupekuliwa, watuhumiwa walikutwa na nyara hizo (vipande vinne vya meno ya tembo) ambavyo vina uzito wa kilogram 5 na thamani yake ni Sh 33 milioni,”amesema Kamanda Mpinga.

Kamanda Mpinga amesema taratibu za kisheria dhidi yao zinaendelea kufanyika ili kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi wakati watuhumiwa wakiendelea kuwa mahabusu.

Hata hivyo, uongozi wa Chuo cha SAUT-Mbeya ulisema jana kwamba mtu huyo anayedaiwa kuwa ni mwanafunzi wao kwa sasa si mwanafunzi wao kwani tangu kuanza muhula wa masomo wa mwaka 2017/2018 hajafika chuoni hivyo hayupo kwenye orodha ya waliosajiliwa chuoni hapo.

“Ni kweli mtu mwenye jina hilo aliwahi kuwepo huko nyuma, lakini wakati tunasajili wanafunzi mwaka wa 2017/2018  huyo mtu sisi hatukumsajili na wala hakuripoti chuoni hapa. Hivyo chuo hakimtambui kama ni mwanafunzi wetu, kwa sababu chuo kina utaratibu kwamba kila muhula ni lazima mwanafunzi asajiliwe upya bila kufanya hivyo na pasipokuwa na maelezo yoyote huwezi kutambulika chuoni”. Amesema Dk.Venancy

Mbali na hilo, Dk. Venancy amesema hata angekuwa ni mwanafunzi wa chuo hicho isingeweza kumpa uhalali wa kutenda kosa hilo kwani chuo hakifundishi uhalifu hivyo hiyo ni tabia ya mtu binafsi na ni mhalifu kama wahalifu wengine, chuo hakiwezi kuingilia kwa lolote lile.