Wizara ya Afya yaajiri wafanyakazi 78 Pemba

Wizara ya Afya Zanzibar imesema jumla ya Wafanya kazi 78  wa kada mbalimbali wanatarajia kuajiriwa Pemba ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi katika wizara hiyo.

Akijibu swali katika kikao cha Baraza la wawakilishi Chukwani,Naibu Waziri wa Wizara hiyo Harusi Saidi Suleiman amesema uajiri huo wa wafanya kazi utasaidia kupunguza tatizo la Uhaba wa wafanyakazi hususan madaktari katika Baadhi ya hospitali na Vituo vya  Afya.

Amesema Serikali inatambua Suala la Uhaba wa Wafanya kazi katika baadhi ya Hospitali na Vituo vya Afya hivyo serikali inaendelea na kufanya utafiti ili kujuwa mahitaji ya wafanya kazi kwa lengo la kuengeza kasi uajiri.

Aidha amesema mbali na Uajiri huo huko Pemba Wizara pia imekusudia kuajiri wafanya kazi hapa Unguja  ili wagonjwa waweze kunufaika na huduma za matibabu.

Amesema Azma ya Serikali ni kuona wananchi wote wananufaika na haki zao za msingi ikiwemo kupata huduma ya Matibabu katika Hospitali na Vituo vya Afya  hivyo ametowa wito kwa Wananchi kuwa wastahamilivu wakati Wizara ikiendelea na Jitihada za kuimarisha huduma za  Afya.

Na;Fat-hiya Shehe Zanzibar24.