Yanga tayari wavalia njuga kuinyaka Bilion 1

Mabingwa wa soka nchini klabu ya Yanga itaanza kibarua cha kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Africa, hatua ambayo itawawezesha kujikusanyia kiasi cha shilingi bilioni 1.1, iwapo wataitoa Township Rollers ya Botswana.

Yanga leo jioni watakuwa wenyeji wa Township Rollers kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam ikiwa ni mechi ya kwanza Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, kuanzia Saa 10:00 jioni.

Kwa mujibu wa utaratibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), timu zinazofuzu hatua ya makundi zinajihakikishia kupata bilioni 1.1 na zinakwenda kuwania fedha zaidi kulingana na matokeo yake kuanzia hatua hiyo.

Kwa timu zitakazofuzu hatua ya Robo Fainali zinajihakikishia kupata shilingi bilioni 1.3 huku zile zitakazofika nusu fainali zinapata shilingi bilioni 1.7 huku bingwa akipata zaidi ya bilioni 2.5 na bingwa akijikusanyia bilioni 3.

Yanga imewahi kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara moja tu, mwaka 1998 katika mfumo wa zamani wa kuanzia hatua ya Robo Fainali, wakati kwenye Kombe la Shirikisho pia ilifika hatua ya makundi mwaka 2016.