Majimaji FC yaonesha kukata tamaakabisa

UONGOZI wa Majimaji FC umesema kuwa, ni Mungu tu ndiye anaweza kuwaokoa kutoshuka daraja kwani kwa jinsi mambo yalivyo, wakiteleza kidogo tu ndiyo kwaheri.

Majimaji ambayo kabla ya mchezo wake wa jana Alhamisi dhidi ya Ndanda FC ilikuwa inaburuza mkia ikiwa na pointi 15 katika michezo 20, inahitaji kupambana vilivyo kuhakikisha haiwi kwenye nafasi mbili za timu ambazo zitashuka daraja mwishoni mwa msimu huu.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Ofisa Habari wa Majimaji, Onesmo Ndunguru alisema: “Kiukweli tunaweza kusema tuna hali mbaya na Mungu pekee ndiye anayeweza kutuokoa na janga la kushuka daraja, hivi sasa tunazipigia hesabu mechi zetu hizi za hivi karibuni ambapo tunahitaji kushinda zote ili kutoka huku chini.

“Haitakuwa rahisi, tuna kazi kubwa ya kufanya ya kupata ushindi mechi hizo ili tuwe sehemu salama, Jumapili tuna mechi dhidi ya Lipuli kwenye uwanja wetu wa nyumbani, hatutakuwa tayari kuona tunashindwa kupata matokeo mazuri nyumbani.”