Mvua yasababisha mnara wa simu kuanguka na kujeruhi Askari Polisi

Jengo  la ofisi ya serikali ya mtaa katika eneo la Goba jijini Dar es Salaam ambalo hutumiwa na polisi, limeangukiwa na mnara wa simu kutokana na mvua iliyonyesha juzi usiku na kumjeruhi askari.
Mvua hiyo ambayo ilianza majira ya jioni ikiambatana na upepo mkali, ilisababisha mnara huo kuanguka na kumjeruhi askari ambaye alikuwa anatoa huduma kwa wananchi katika eneo hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa eneo hilo linalotumika na askari sio jengo lao, bali ni mali ya ofisi ya serikali ya mtaa.
Alifafanua kuwa wakati jengo hilo linaangukiwa na mnara kulikuwa na askari mmoja ambaye alikuwa anatoa huduma za kiusalama katika eneo la Goba na alipata majeraha kadhaa na hali yake inaendelea vizuri.
Alisema askari huyo alikwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na sasa yupo nyumbani akiendelea vizuri.