Mke wa Lissu asimulia upasuaji anaotarajiwa kufanyiwa mumewe

Wakati Tundu Lissu akitarajiwa kufanyiwa upasuaji wa 19 katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven nchini Ubelgiji keshokutwa, mkewe amesema walilitambua hilo tangu wakiwa Nairobi nchini Kenya.

Alicia Lissu alisema hayo alipozungumza na Mwananchi jana baada ya mbunge huyo wa Singida Mashariki kueleza kuwa Jumatano atafanyiwa upasuaji wa mguu wa kulia ili kumwezesha kupona haraka.

Upasuaji huo ni mwendelezo wa aliokuwa akifanyiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikokuwa amelazwa baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa katika makazi yake mjini Dodoma Septemba 7, 2017.

Lissu alipelekwa kwa matibabu jijini Nairobi usiku wa siku aliyoshambuliwa baada ya kupata matibabu ya awali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

“Tulipokuwa Nairobi madaktari walitueleza kutafanyika upasuaji mwingine kwa sababu pale kazi yao ilikuwa kuokoa maisha yake na kuweka mwili wake sawa kutokana na majeraha aliyokuwa amepata,” alisema Alicia.

“Upasuaji kwa mguu wa kulia ni kitu walichotueleza, walituandaa na hata tulipofika hapa madaktari wakataka kujiridhisha kwa kufanya vipimo kuangalia mwili wake utakuwaje kipindi cha mazoezi maalumu.” Alisema walifanya vipimo kuona uwezo wa mguu na hasa juu ya goti na wamejiridhisha kuwa ana maendeleo mazuri ya mazoezi na ana imani baada ya upasuaji ataendelea vizuri zaidi.

Alicia, ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema katika majuma yaliyopita Lissu aliruhusiwa kutoka hospitalini na alikuwa akienda kwa ajili ya mazoezi tu. Akizungumzia maendeleo ya Lissu kiafya, Alice alisema: “mwanzo niliwaza hataamka lakini ameamka, nina furaha sana amekuwa na maendeleo mazuri kwa miezi miwili tukiwa hapa.”

“Kutoka kitandani na kufikia hatua ya kusimama, kuanza kujihudumia ni hatua kubwa, nina furaha, namshukuru Mungu amesikia maombi yetu na ya wengine na hii ni faraja kwetu,” alisema.

Alicia alisema Lissu ambaye pia ni rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amekumbuka harakati zinazoendelea nchini akisema akipona anataka kurudi nyumbani ashiriki kupigania utawala bora.

Alisema baadhi ya wanaomtembelea Lissu wamekuwa wakimshauri akirejea nyumbani asirudi katika mazingira yatakayohatarisha maisha yake.

Lissu juzi alitoa taarifa ya maendeleo ya afya yake akisema anaweza kusimama bila msaada na amejuzwa na timu ya madaktari kuwa kasi ya mfupa wa juu ya goti kuunga ni ndogo.

“Madaktari wangu wamesema wasipoingilia kati na kurekebisha mfupa huo itachukua muda mrefu sana kuunga,” alisema.

Alisema madaktari wamemweleza hata mfupa huo ukiunga baada ya muda mrefu, hautaunga kwa namna utakayoondoa hatari ya kuvunjika baadaye.

“Kwa sababu hizi, madaktari wangu wamependekeza kufanya operesheni nyingine kwenye mfupa wa juu ya goti la kulia, Machi 14 nitarudi Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg kwa ajili ya kufanyiwa operesheni hiyo,” alisema.

Alisema yuko katika mikono salama ya kitabibu chini ya madaktari Profesa Stefa Nijs na Profesa Willem-Jan Mertsemakers ambao ni madaktari bingwa wa mifupa wanaosifika barani Ulaya.

“Hivyo, msiwe na hofu. Mungu wetu aliyeniwezesha kuwa hai sasa, ataendelea kutenda miujiza kupitia kwa madaktari bingwa hawa,” alisema.