Rais Magufuli ataja sababu ya kuto safiri nje ya nchi

Akiwa ametimiza siku 859 madarakani, Rais John Magufuli ametembelea nchi chache huenda kuliko watangulizi wake wanne.

Magufuli ametembelea Kenya, Uganda, Rwanda na Ethiopia katika kipindi chote cha utawala wake huku akitimiza miaka miwili, miezi minne na siku saba tangu aapishwe kuwa Rais wa Tanzania Novemba 5, 2015.

Huenda hilo lilimfanya jana atoe siri na sababu zinazomfanya asipende kusafiri mara kwa mara nje ya nchi.

Akiwa mjini Singida jana alikozindua kiwanda cha mafuta ya kupikia cha Mount Meru Millers Group, Rais Magufuli alisema amekataa zaidi ya mialiko 70 ya kwenda nje ya nchi kwa sababu hakuchaguliwa na Watanzania kwenda huko bali kuwatumikia.

“Nataka Tanzania yote niizungukie ndiyo maana sitaki kwenda nje, maana huko si kwenye jimbo langu, jimbo langu mimi ni Tanzania. Nimekataa mialiko zaidi ya 70. Niende nje kufanya nini wakati sijamaliza kutatua kero za wananchi.”

“Nataka nizitatue kero za wananchi walionipigia kura kwanza, walipanga foleni wakati wa mvua na jua kunichagua mimi na waheshimiwa wabunge,” alisema Rais Magufuli.

Bado sijaenda, Iringa, Mbeya, Rukwa na sehemu nyingine, lazima nizunguke nchi yote kutatua kero za wananchi..” alisema.