SMZ yahimizwa kuandaa mbinu bora ili wananchi kuweza kujiajiri

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetakiwa kuwaandalia mazingira ya kuweza kujiajiri wananchi wa Ukongoroni na Charawe ili waachane na tabia ya uharibifu wa mazingira unaosababisha athari mbali mbali ikiwemo maji ya chumvi kuingia katika mashamba ya kilimo.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa kamati ya Mazingira Ukongoroni Fadhil Sudi wakati akizungumza na Zanzibar24, amesema licha ya elimu inayotolewa juu ya athari za Uharibifu wa mazingira lakini wananchi wamekuwa wagumu kuachana na tabia hiyo kwa kisingizio cha kutokuwa na shughuli za kuwaingizia kipato cha kujikimu na familia zao.

Amesema serikali itakapo kaa pamoja na wananchi hao  ili kuwasaidia namna ya kuweza kujiajiri itazuia athari za uharibifu wa mazingira zinazofanywa na baadhi wa watu kijijini hapo ikiwemo ukataji wa mikoko katika fukwe za bahari.

 

Kwa upawe wao wananchi wa vijiji hivyo wamesema wapotayari kuachana na tabia ya ukataji wa miti ya mikoko pindipo watapopatiwa elimu ya kuweza kujiajiri katika sekta mbali mbali ikiwemo kilimo na ufugaji.

Wamesema mpaka sasa wamejiunga katika vikundi mbali mbali vya kuweka na kukopa lakini havikidhi mahitaji yao kutokana na maslahi madogo wanayoyapata na kusababisha vikundi vyengine kutofikia malengo waliyoyakusudia.

 Aidha wametowa wito kwa viongozi wa majimbo na Serikali kuwasaidia wataalamu wa kilimo na Ufugaji ili waweze kujiunga na kilimo cha kisasa ambacho kitaweza kuwapunguzia ugumu wa maisha na pamoja na kuweza kuachana na Ukataji wa miti ovyo.

 

Nae katibu tawala wa Wilaya ya Kati Omar Abdallah Juma amesema tayari serikali imekusudia kukaa na wananchi hao na kuwapa elimu ya ufugaji hususani ufugaji wa nyuki ili kuondokana na tabia ya uharibifu wa mazingira.

Aidha amewata wananchi hao kutumia rasilimali za bahari ikiwemo  kufuga majongoo na kaa ili waweze kunufaika na mazao ya baharini vijijini mwao .

Katibu tawala huyo ametowa wito kwa kamati za ulinzi wa Mazingira kuendelea kushajihisha wananchi kuachana na ukataji wa miti kinyume na sheria pamoja na kuwaripoti katika vyombo vya sheria wananchi wanaoharibu mazingira kwa maksudi.

 Na;Fat-hiya Shehe Zanzibar24.